577 wajitokeza kupima VVU Tanga

  • Viongozi mbalimbali na wakazi wa Jiji la Tanga wakiwa katika viwanja vya usagara vilivyopo jijini Tanga ambapo shughuli mbalimbali zimefanyika kiwemo upimaji wa vvu na chanjo ya  UVIKO 19.

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkesha wa mwaka mpya, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa amesema katika watu 577 waliopima VVU wanawake walikuwa 372 na wanaume 202 huku waliokutwa na maambukizi wakiwa watatu sawa na asilimia 0.51.

Tanga. Watu 577 wamepimwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliowasili mkoani Tanga jana ukitokea Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Ukiwa mkoani hapa, Mwenge umekagua na kuzindua miradi saba ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanga Mjini yenye thamani ya Sh20.037 bilioni.

Akitoa takwimu za upimaji wa VVU, Uviko-19 na malaria katika mkesha huo leo Mei 27, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa amesema katika watu 577 waliopima VVU wanawake walikuwa 372 na wanaume 202 huku waliokutwa na maambukizi wakiwa watatu sawa na asilimia 0.51.

"Aidha, kuna waliopimwa malaria hawa walikuwa 161 na waliokutwa na maambukizi ni wanne na waliochanja chanjo ya Uviko-19 walikuwa 443 lakini pia tulikuwa na shughuli ya uchangiaji wa damu ambapo watu tisa walijitolea," amesema DC Mgandilwa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Geraruma amewataka wananchi mkoani Tanga kuzingatia ujumbe wa mwenge kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.

"Mwenge pia unawakumbusha kuzingatia afya njema kwa kupata lishw bora, mapambano dhidi ya malaria, dawa za kulevya na kupiga vita rushwa," amesema.

Mwenge wa Uhuru leo utakuwa katika Wilaya ya Mkinga.