64 wapatiwa uraia wa Tanzania, 17 waukana
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.
Muktasari:
- Wizara hiyo kupitia Idara ya Uhamiaji imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu maombi ya uraia kwa wageni wanaotaka kuwa raia wa Tanzania pamoja na Watanzania wanaokana uraia wao kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 ya mwaka 2023.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, wageni 64 walipewa uraia wa Tanzania huku Watanzania 17 wakikana uraia wao baada ya kupata uraia wa mataifa mengine.
Pia amesema Watanzania 229 walizuiwa kuondoka nchini kutokana na kutokidhi vigezo vya kusafiri nje ya nchi, wakati Watanzania 203 walirejeshwa kutoka mataifa mbalimbali kwa kukiuka sheria za nchi husika, ikiwemo kuingia na kuishi bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Amesema hayo leo Jumatatu, Mei 25, 2026 bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Katambi amesema wizara hiyo kupitia Idara ya Uhamiaji imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu maombi ya uraia kwa wageni wanaotaka kuwa raia wa Tanzania pamoja na Watanzania wanaokana uraia wao, kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 ya mwaka 2023.
"Idara ya Uhamiaji imeendelea kuwezesha na kudhibiti huduma za kiuhamiaji kwa Watanzania wanaosafiri kuingia na kutoka nchini kwa shughuli mbalimbali.”
“Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Watanzania 476,190 waliondoka nchini na 443,561 kurejea, ikilinganishwa na Watanzania 400,434 waliotoka na 376,011 waliorejea katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25," amesema.
Kwa upande wa nyaraka za usafiri, amesema pasipoti 78,583 zilitolewa kwa Watanzania katika kipindi hicho. Kati ya hizo, 555 zilikuwa za kibalozi, 258 za kiutumishi na 77,770 za kawaida. Idadi hiyo ni pungufu ikilinganishwa na pasipoti 114,448 zilizotolewa mwaka 2024/25.
"Vilevile, hati za safari za dharura 226,400 zilitolewa katika kipindi hicho, ikilinganishwa na hati 204,387 zilizotolewa mwaka uliotangulia," amesema Katambi.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Idara ya Uhamiaji itaendelea kutoa pasipoti na hati nyingine za safari ili kuwawezesha Watanzania kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali.
Kuhusu udhibiti wa uhamiaji haramu, Katambi amesema hadi kufikia Aprili 2026, watuhumiwa 49,469 wa makosa ya kiuhamiaji walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ambapo wahamiaji haramu 34,099 waliondoshwa nchini.
Amesema wizara kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha Kanda Maalumu za Uhamiaji katika mikoa ya Kagera na Kigoma kwa lengo la kudhibiti wahamiaji haramu, hasa katika maeneo ya mipakani, kwa kuongeza askari pamoja na vitendea kazi.
Amesema operesheni, misako na doria zitaendelea pamoja na kuanzishwa kwa kanda nyingine katika maeneo ya kimkakati yenye mwingiliano mkubwa wa wageni.
Katika suala la wakimbizi na waomba hifadhi, Katambi amesema waomba hifadhi wapya 1,214 walipokewa na kusajiliwa kati ya Julai 2025 hadi Aprili 2026.
Waomba hifadhi hao walitoka katika mataifa mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan, Sudan Kusini, Kenya, Ethiopia, Eritrea, Uganda, Egypt, Syria, Afghanistan, Pakistan, Ukraine na Yemen.
Amesema hadi Aprili 2026, Tanzania ilikuwa ikihifadhi wakimbizi na waomba hifadhi 158,954, ambapo 70,952 walikuwa na asili ya Burundi, watu 87,303 walitoka DRC na 699 walitoka mataifa mengine.
Kwa upande wa mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, Katambi amesema wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya operesheni za kuwaokoa waathirika na kuwakamata wahusika wa uhalifu huo.
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, waathirika 160 waliokolewa na kusaidiwa, ambapo 60 walikuwa watoto, 96 wanawake na wanne wanaume. Kati yao, waathirika 126 waliokolewa nchini, huku wengine 34 wakiokolewa kutoka mataifa ya Bahrain, India, Malaysia, Egypt, Oman, Syria na United Arab Emirates.