76 mbaroni wakidaiwa kumpiga mkuu wa kituo cha polisi
Muktasari:
- Polisi mkoani Rukwa, inawashikilia watu wapatao 76 kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi Mkuu wa Kituo cha Polisi Kabwe, kilichopo wilayani Nkasi na kuharibu mali mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
Sumbawanga. Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 76 kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi Mkuu wa Kituo cha Polisi Kabwe, kilichopo wilayani Nkasi na kuharibu mali mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Shedrack Masija ameiambia Mwananchi Digital kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 11, 2023 ambapo kundi la watu zaidi 20, walivamia Kituo cha Polisi na kumpiga mkuu wa kituo hicho na kuchoma moto uzio, kubomoa madirisha, kuharibu pikipiki mbili na kuharibu samani mbalimbali za kituo hicho.
Amesema chanzo cha kurugu hizo ilikuwa ni wananchi kumshinikiza mkuu wa kituo hicho awaachilie huru watuhumiwa wanane waliokuwa wamekamatwa na polisi, usiku wa Septemba 10, 2023 kwa kosa la kuchangisha fedha wananchi ili kuwaleta watu wanaodaiwa kujifanya waganga wa kienyeji (Lambalamba), wenye uwezo wa kuwabaini na kuwakamata wachawi.
Kamanda huyo amesema kuwa baada ya wananchi kuvamia kituo hicho na kubaini watuhumiwa hao hawapo kituoni hapo, walivamia baadhi ya maduka, nyumba za kulala wageni na kupora bidhaa mbalimbali kama vile magodoro, mafuta ya diezeli, petroli, mafuta ya taa, friji, magunia ya mpunga, simenti, Tv, makochi, mabati na bidhaa nyingine za madukani.
Inaeelezwa kuwa pia waliwashambulia wale wote waliowatuhumu kuwa ni wachawi, vile vile walivunja madirisha ya zahanati ya kijiji, ambapo baada ya saa kadhaa za kufanyika kwa vurugu hizo, Polisi walipata taarifa na kufika kwenye eneo hilo, ambapo walikuta gari la mkuu huyo wa kituo limevunjwa vioo vyote.
Kamanda Masija pamoja na kulaani vikali vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, lakini pia ameowaonya wananchi kuacha kuwakumbatia ‘lambalamba’ kwa kuwa, kufanya hivyo kuna hatarisha uvunjifu wa amani kutokana na watu hao kufanya lamli chonganishi.
Amewataka wale wote waliopora mali za wananchi kuzisalimisha Polisi kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika walihusika na vurugu hizo.
Hata hivyo uchunguzi wa mwandishi wa gazeti hili umebaini kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baadhi matajiri wa Kijiji cha Kabwe kutumia nguvu ya fedha kuzuia lambalamba kufanya kazi yao ya kuwafichua wachawi.
Kamanda huyo alisema watuhumiwa wote waliokamatwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.