Viongozi CCM wakamatwa kwa tuhuma za kumpiga polisi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga

Muktasari:

  • Katibu wa CCM Wilaya ya Babati, Filbert Mdaki (52) na Katibu wa jumuiya ya vijana UVCCM wa wilaya hiyo, George Sanka (46) wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga askari polisi mateke na fimbo.

Babati. Katibu wa CCM Wilaya ya Babati, Filbert Mdaki (52) na Katibu wa jumuiya ya vijana UVCCM wa wilaya hiyo, George Sanka (46) wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga askari polisi mateke na fimbo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea kijiji cha Kirudiki wilayani Babati Desemba 16 saa 11 jioni.

Kamanda Kuzaga alisema watuhumiwa hao walimshambulia Koplo Baraka wa Kituo kidogo cha Polisi Kiru kwa kwa mateke na fimbobaada ya kufika kwenye mkusanyiko wa wananchi wa Kijiji cha Kirudiki.

“Askari huyo baada ya kuona mkusanyiko alifika ili aulizie juu ya kibali cha mkusanyiko huo, ndipo viongozi hao wakamshambulia maeneo mbalimbali ya mwili,” alisema kamanda Kuzaga.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Kada wa CCM wa mjini Babati mkoani Manyara, Cosmas Masauda, ameeleza kusikitishwa kwa kitendo cha viongozi hao kukamatwa na kupelekwa mahabusu wakiwa kazini.

Masauda alisema mkutano huo ulikuwa na kibali na viongozi hao walikwenda kwa ajili ya kuzungumzia mgogoro wa shamba baina ya wanakijiji na mwekezaji.

Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara, Simon Lulu alisema atazungumzia jsuala hilo baada ya ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumalizika.

“Tumepanga kuwa baada ya ziara ya

 Waziri Mkuu Majaliwa ndipo tutazungumza juu ya tukio hilo la viongozi wetu kukamatwa,” alisema Lulu.