Prime
ACT Wazalendo: NEC ijiuzulu, Tume mpya iundwe
Muktasari:
- Miezi michache baada ya Bunge kupitisha muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, ACT-Wazalendo leo Jumapili Machi 24, 2024 imetoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya sasa kujiuzulu kupisha kuundwa mpya itakayopatikana kwa utaratibu wa ushindani.
Dar es Salaam. Miezi michache baada ya Bunge kupitisha muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, ACT-Wazalendo leo Jumapili Machi 24, 2024 imetoa wito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya sasa kujiuzulu kupisha kuundwa mpya itakayopatikana kwa utaratibu wa ushindani.
Chama hicho kimetoa wito huo baada ya kueleza kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Machi 20, 2024 katika kata 22 nchini pamoja na mwingine uliofanyika tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani.
ACT-Wazalendo inaeleza katika uchaguzi mdogo uliofanyika hauna tofauti na uliofanyika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hivyo inapendekeza kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria Mpya ya Tume ya Uchaguzi.
Februari 2, mwaka huu, Bunge lilipitisha miswada mitatu ya sheria za uchaguzi ikiwamo Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na marekebisho yake yaliyofanywa na wabunge kwenye baadhi ya vifungu vya sheria hiyo.
Takribani miezi miwili imepita tangu sheria hiyo ilipopitishwa na Bunge, huku Tume na wanasheria wakifafanua hatua za sheria kuanza kutumika.
Wakati ACT-Wazalendo ikilalamikia rafu kwenye uchaguzi huo, Machi 5, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana aliwahakikisha Watanzania kwenye mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo kwamba Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka huu na ujao uwe huru na wa haki.
Wailaumu Tume ya Uchaguzi
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Issihaka Mchinjita, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ameeleza malalamiko ya chama hicho kuhujumiwa kwenye uchaguzi huo kutokana na kukosekana kwa Tume Huru hasa baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo.
Mchinjita amedai Tume ya Uchaguzi ilihusika kugawa karatasi za kupigia kura kwa makada wa CCM ili wazitumbukize kwenye masanduku ya kura. Amedai jambo hilo lilifanyika kwenye kata zote zilizofanya uchaguzi.
Mchinjita amedai kuwa, jitihada za viongozi wa ACT-Wazalendo kuripoti suala hilo kwa maofisa wa Tume ya Uchaguzi hazikusaidia kitu kwa kuwa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Amedai kuwa, viongozi waliojaribu kuwadhibiti makada wa CCM kutumbukiza kura hizo kwenye masanduku walikabiliwa na Jeshi la Polisi.
“Kwa vile muundo na utaratibu mpya umepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Tume ya sasa ijiuzulu yote kupisha kuundwa kwa Tume mpya itayopatikana kwa utaratibu wa ushindani,” amesema Mchinjita.
Kiongozi huyo wa alisema ni muda mwafaka kwa Tume ya Uchaguzi kuwa na watumishi wake hadi katika ngazi ya halmashauri ili uchaguzi usisimamiwe na watumishi wa halmashauri ambao wengi alidai ni makada wa CCM.
Majibu ya Tume
Alipotafutwa kuzungumzia wito wa ACT-Wazalendo wa kujiuzulu kwa Tume hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu kwa Mpigakura wa NEC, Giveness Aswile amesema kila jambo lina utaratibu wake.
Amesema Tume haina shida isipokuwa inasubiri maelekezo.
“Tume ni taasisi inayopewa taarifa, haiwezi kuamua kusema leo asubuhi naondoka, sheria mpya ina taratibu zake, sisi hatuwezi kusimamisha shughuli, isipokuwa tunaendelea na sheria iliyopo hadi tupewe nyingine na itangazwe,” amesema Aswile.
Amesema wadau hao (ACT-Wazalendo) wasilalamike kama hawajui, akieleza hata wao wanawategemea wawasaidie kwa sababu wana masilahi na sheria hiyo.
“Tume ni refa tu, lakini kuna timu zinazoshiriki kwenye mashindano na makamisaa, bahati mbaya Tume ni refa wa kudumu tofauti na marefa wa uwanjani, kwa hiyo na sisi tunasubiri sheria mpya,” amesema Aswile.
Amewaomba ACT-Wazalendo kuwa watulivu wakati michakato ya sheria mpya ukiendelea, akieleza Tume haina shida wala haiwezi kung’ang’ania, bali wanasubiri maelekezo.
Kuhusu malalamiko ya kura, alisema bado hawajapokea ripoti kwa kata zote ambazo uchaguzi mdogo umefanyika, hivyo itakuwa vigumu kuzungumzia.
“Tunategemea kuanzia kesho (leo) halafu tutafanya tathimini na kuzungumzia kilichotokea baada ya kupokea ripoti zote na kuziangalia,” amesema Aswile.
Msimamizi wa uchaguzi katika Kata ya Chiputa, iliyopo Halmashauri ya Nanyamba, Ibrahim Mwanauta alisema katika kituo alichosimamia uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki, ndiyo maana ulimalizika kwa usalama.
“Kituo nilichosimamia tulimaliza salama, hakuna sehemu yoyote iliyoleta shida, sasa sijajua kama kulikuwa na shida nyingine lakini kama msimamizi wa uchaguzi ulikuwa huru na haki,” amesema Mwanauta.
Wanasheria wafafanua
Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Haki Kwanza, Alloyce Komba alisema sheria mpya itaanza kufanya kazi baada ya kusainiwa na Rais Samia, ingawa kuna sheria zingine zinasema hadi waziri achapishe kwenye gazeti la Serikali na atunge kanuni ndipo ianze kutumika.
“Siku Rais akisaini inaanza kazi, waziri na mamlaka husika watasema inaanza lini kufanya kazi, lakini kama sheria itakuwa inataka kuundwa kwa vyombo mbalimbali ikiwamo bodi inajumuishwa kwenye kanuni,” amesema Komba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumzia sheria hiyo hiyo alisema, “binafsi hadi saa hizi sijaona kama imesainiwa, ingesainiwa ningejua lakini hizi sheria mpya hazitasaidia kupunguza au kuongeza chochote kwa sababu mabadiliko yamekuwa madogo, ni sawa na asilimia 20 tu,” amesema Anna.
Amesema kwa asilimia 80 bado zimebakia zilezile kwa sababu Katiba haikuguswa lakini ingeguswa mabadiliko makubwa yangetokea na ingeleta mwanga kwa Tume ya Uchaguzi.
“Tume iliyopo sasa bado ni halali kwa sababu sheria mpya bado haijaja, hadi isainiwe nyingine ndipo yatatokea ya mabadiliko,” amesema.
Tuhuma dhidi ya polisi
Mchinjita amedai Jeshi la Polisi lilitumia mabavu kuwakamata viongozi wa ACT-Wazalendo katika tukio lililofanyika kwenye Halmashauri ya Kigoma Ujiji kwenye Kata ya Kasingirima wakati wakizuia kura feki zisiingizwe kwenye masanduku.
Amewataja waliokamatwa kuwa Abdul Nondo (Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa), Karama Kaila (mjumbe wa Kamati Kuu Kanda ya Magharibi), Selemani Simba (mwenyekiti wa Ngome ya Wazee mkoa wa Kigoma), Alumbula Khalidi (mgombea udiwani kata ya Kasingirima) na wanachama Ntakije Ntanena na Khamis Mzungu.
Akijibu tuhuma hizo, Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime amesema majukumu ya chombo hicho yapo kisheria ikiwamo kulinda maisha ya watu na mali zao, kubaini na kuzuia uhalifu, kusimamia sheria na kulinda amani na si kulumbana na mtu yeyote.
“Kama kuna mtu yeyote yule mwenye malalamiko yenye ushahidi afuate sheria kama inavyoelekeza ili tuhuma hizo zichunguzwe. Pia, kama kuna malalamiko juu ya uchaguzi sheria inaelekeza ni nini cha kufanya na si kujenga chuki katika jamii,” amesema Misime.
CCM yajibu
Akijibu tuhuma zilizotolewa na Mchinjita, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema sheria za nchi zipo wazi, kama wanahisi mambo hayakwenda vizuri waende mahakamani na si vinginevyo.
“Sheria inasema unaenda mahakamani kama una ushahidi, ukiona mtu hataki kufuata utaratibu anaenda kufanya mkutano na vyombo vya habari maana yake mambo anayoongea ni ya kutunga na mimi siwezi kusimama kujibu mambo ya kutunga,” amesema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi amesema alishawahi kupelekwa mahakamani kwenye uchaguzi wa ubunge na mpinzani wake ambaye baadaye alishindwa kesi na alitakiwa kumlipa lakini yeye alitumia busara akamsamehe.
“CCM matumaini yetu waliochaguliwa walifanya kampeni kistaarabu na wale wenye wasiwasi wafuate taratibu za kisheria, wakiendelea kupiga kelele wanataka huruma.”
Mbunge Chadema afunguka
Akitoa tathimini ya uchaguzi kwenye Kata ya Kabwe iliyopo Jimbo la Nkasi Kaskazini, mbunge wa jimbo hilo (Chadema), Aida Kenani alisema mambo yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 bado yanaendelea kwa kilichotokea kwenye kata hiyo.
“Wananchi walitimiza wajibu wao wa kupiga kura na mgombea aliyewekwa kupitia ACT-Wazalendo alishinda kwa ushahidi kabisa, kilichofanyika ni uporaji na kinanyong’onyesha Watanzania umuhimu wa kwenda kupiga kura,” amedai.