ACT-Wazalendo: Serikali iongeze mabasi ya mwendokasi njia ya Kimara

Muktasari:
- Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amekosoa upungufu wa mabasi ya UDART na kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kutatua kero ya usafiri.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kivuli wa chama cha ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amesema uendeshaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) unakumbwa na changamoto kubwa, hasa kutokana na upungufu wa mabasi unaoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Magomeni, muda mfupi baada ya kuachiwa na polisi alipokamatwa wakati akisikiliza changamoto za wasafiri, alipofanya ziara kama abiria wa kawaida kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Awali, kiongozi huyo alikamatwa na askari wa Polisi katika kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Kimara, na kupelekwa Kituo cha Polisi Mbezi Magufuli, ambapo alizuiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa bila masharti yoyote.
Mchinjita amesema amejionea hali halisi ya usafiri wa umma, na kuishauri Serikali kuacha kuficha ukweli kuhusu changamoto hizo na kuchukua hatua madhubuti za kutatua kero zinazowakabili wananchi.
“Wiki mbili zilizopita tulifanya uchambuzi wa Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilionyesha yapo matatizo katika DART hasa ukosekanaji wa magari, CAG alionyesha kati ya mabasi 210 yaliyotolewa kwa ajili ya mradi, mabasi 99 hayafanyi kazi,” amesema.
“Naitaka Serikali izingatie kuwa tatizo la mwendokasi ni tatizo walilojitengenezea wenyewe, waliondoa utaratibu wa kutumia daladala na kuwalazimisha wananchi kutumia mabasi haya. Tumefanya uwekezaji mkubwa ambao ulilenga kumpunguzia mtu muda wa kufika mjini hadi dakika 45. Utamaduni huu umezoeleka, hivyo Serikali ichukue hatua za haraka na za muda mrefu,” amesema.
Akizungumzia suala hilo alipozungumza na Mwananchi, Msemaji wa UDART, Gabriel Katanga, ameeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuondoa changamoto ya uhaba wa magari na kwamba baada ya miezi mitatu, mabasi 100 yanatarajiwa kuwasili ili kuanza kutoa huduma.
“Kwa sababu basi moja la mfano liliingia Aprili (tayari limeingia) kati ya hayo 100 yaliyobaki 99 yatawasili nchini baada ya miezi mitatu,” amesema.
Amesema mabasi hayo yamekusudiwa kuboresha huduma za usafiri katika awamu ya kwanza ya mradi huo inayohusisha barabara ya Morogoro, na yote yatatumia mfumo wa gesi.
Awamu hiyo ya kwanza ya mradi inajumuisha barabara za Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni, Kimara-Gerezani na Kimara-Morocco.
Mradi huo ulianza kutoa huduma mwaka 2016 baada ya kuzinduliwa na Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli.
Sambamba na hayo, Katanga amesema kuwa kasoro ya awali katika injini ya mabasi hayo imetatuliwa.
“Yale ya awali yalikuwa na injini nyuma, hivyo yaliingiza uchafu; haya mapya yameboreshwa, na ingawa .injini bado zipo nyuma, tatizo hilo halitatokea tena,” amesema.
Ushauri wake
Mchinjita amesema eneo la Kimara, lenye abiria wengi, linapaswa kupewa kipaumbele kwa kupelekewa magari zaidi, hata kama ni kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani kutoa magari ya muda ili kutatua kero hiyo.
Amesema si sahihi kwa wananchi kukatishwa tiketi, kisha wakalazimika kusubiri muda mrefu vituoni, kwani hata wakati daladala zilikuwepo, tatizo hilo halikuwepo.
“Pia, Serikali iangalie namna bodi ya UDART inavyoendeshwa. Inaonekana wanatumia nguvu kubwa kuzuia kujulikana kwa kero zilizopo. Wao ndio waliokabidhiwa mabasi 210 na sasa hayapo,” amesema.
Alivyokamatwa
Amesema alifanya safari kama abiria wa kawaida, na alipoanza kusikiliza changamoto za wananchi, watumishi wa mradi huo walimtaka asitishe, muda mfupi baadaye alianza kufanyiwa fujo.
Baada ya mzozo huo, ameeleza kuwa watumishi hao waliwaita askari Polisi ambao walikwenda kumkamata pamoja na waandishi wa habari na wanachama waliokuwa katika eneo hilo.