ACT Wazalendo wataka TICTS isitishiwe mkataba

Msemaji wa Sekta ya Mawasiliano,Teknolojia,Habari na Uchukuzi chama cha ACT Wazalendo, Ally Saleh akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam,kuhusu utendaji kazi wa kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumu  Makontena Tanzania (TICTS). Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

ACT wameitaka Serikali kuiwezesha TPA kusimamia kitengo cha makasha cha bandari ya Dar es Salaam katika wakati wa mpito ambapo itakuwa kwenye mchakato wa kutafta mwekezaji mwingine.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha mkataba na kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS) katika bandari ya Dar es Salaam kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kikidai kuwa kampuni hiyo haina utendaji wa kuridhisha.

Mapendekezo hayo yamekuja wakati mkataba wa TICTS iliyofanya kazi katika bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2000, ukiwa unaelekea ukingoni na bado haijawekwa wazi kama watapewa mkataba mwingine.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21 jijini hapa, msemaji wa sekta ya mawasiliano, teknolojia, habari na uchukuzi wa ACT Wazalendo, Ally Salehe suala la ukodishwaji au kutokodishwa tena TICTS linapaswa kuchukiliwa na lifanyiwa maamuzi kwa uzalendo mkubwa.

“Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na kampuni binafsi ya kimataifaya kuhudumia makontena (TICTS), kwa kuwa ni wazi imeshindwa kukidhi matarajio ya kukodisha kwake,” amesema Salehe.

Vilevile ACT wameitaka Serikali kuiwezesha TPA kusimamia kitengo cha makasha cha bandari ya Dar es Salaam katika wakati wa mpito ambapo itakuwa kwenye mchakato wa kutafta mwekezaji mwingine.

“Serikali ifanye uchambuzi wa kina katika kutoa zabuni kwa kampuni zenye sifa ya kimataifa kupitia TICTS kwenye utendaji wake mzima wa miaka 20 na faida zake na uwezo wa kufikisha malengo mapya ya mkataba wao,” amesema.

Pia ACT imeitaka Serikali kuongeza usimamizi wa wa suala hilo ili kuongeza ufanisi.

“kwa kuwa imetajwa kuwa moja ya kilichochangia hali ya sasa ni kuwa Serikali haikuwekeza ipasavyo kwa yale inayowajibika nayo, nbi vema jambo hilo lisimamiwe kwa umuhimu mkubwa ili kuongeza ufanisi,” amesema.