ACT-Wazalendo yatilia shaka mpango wa hadhi maalumu kwa diaspora
Muktasari:
- ACT- Wazalendo imesema hadhi maalumu ni mbinu ya kukwepa uraia pacha kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hadhi maalumu iliyotangazwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Watanzania waishio nje ya nchi, ni mbinu ya kukwepa uraia pacha kwa Watanzania.
Chama hicho kimesema tamko lililotolewa na waziri wa wizara hiyo, January Makamba, Desemba 17, 2023 chama hicho kimesema wasiwasi wake ni kwamba uamuzi uliotangazwa ni wa kienyeji tu ili kusahaulisha mpango wa uraia pacha.
“ACT-Wazalendo tunasisitiza, haitoshi kufanya marekebisho ya sheria za uhamiaji kwa kuzingatia mambo machache, bali tunashinikiza uraia pacha kama suluhisho la uhakika,” kimesema chama hicho katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya msemaji leo Desemba 20,2023.
ACT-Wazalendo imesema inatambua umuhimu wa Watanzania waliotawanyika kote duniani kama sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa.
“Kwa kutambua umuhimu wao, wito wa uraia wa nchi mbili ni wa muhimu si tu kama upendeleo, bali kama hitaji la kimsingi linalotokana na utambuzi wa michango yao na ustawi wa Tanzania,” imesema taarifa hiyo.
Chama hicho kimesema uraia pacha ndiyo suluhu inayofaa zaidi na kuthibitisha kwamba, uhusiano wa Watanzania waishio nje na Taifa lao la asili bado haujavunjwa na unathaminiwa.
“Tunakubali ukweli kwamba michango yao katika ukuaji na maendeleo ya Tanzania haibanwi na mipaka inayoonekana. Tunaamini uraia pacha ni njia itakayowawezesha kusafiri bila vikwazo, kufungua njia za ushirikiano wa kiuchumi, kubadilishana ujuzi na kuimarisha utamaduni,” kimesema.
ACT-Wazalendo imesema uraia wa nchi mbili si tu mabadiliko ya sera, bali ni hatua ya kimkakati kuelekea kujenga Taifa lenye nguvu, lililounganishwa zaidi.