ACT yaeleza sababu Ticts kutopewa mkataba mpya

Msemaji wa Sekta ya Mawasiliano,Teknolojia,Habari na Uchukuzi chama cha ACT Wazalendo, Ally Saleh akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam,kuhusu utendaji kazi wa kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumu  Makontena Tanzania (TICTS). Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Wakati Serikali ikiendelea na mazungumzo na kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS) kuhusu kuipa mkataba mwingine, Chama cha ACT -Wazalendo kimeitaka Serikali kutoongeza mkataba na kampuni hiyo inayofanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam, kikidai kuwa haina utendaji wa kuridhisha.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na mazungumzo na kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS) kuhusu kuipa mkataba mwingine, Chama cha ACT -Wazalendo kimeitaka Serikali kutoongeza mkataba na kampuni hiyo inayofanya kazi katika Bandari ya Dar es Salaam, kikidai kuwa haina utendaji wa kuridhisha.

Mapendekezo hayo yamekuja wakati mkataba wa TICTS, iliyofanya kazi katika bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2000, ukiwa unaelekea ukingoni na bado haijawekwa wazi kama watapewa mkataba mwingine au la.

Akizungumza kwa simu na gazeti la The Citizen ambalo ni gazeti dada la Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Gabriel Migire alisema Serikali bado iko kwenye majadiliano na TICTS ili kuona kama iendelee na mkataba au isiendelee.

Alisema kitu cha msingi kwa Serikali ni kuhakikisha inalinda masilahi ya Watanzania katika mradi huo unaolenga kuongeza ufanisi katika bandari hiyo.

“Timu yetu ya wataalamu iliyoundwa na Serikali bado ina muda wa kutosha wa kujadiliana na TICTS na hatimaye tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuamua kama tunaingia mkataba mwingine au hapana,” alisema Migire.


Kauli ya ACT- Wazalendo

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Msemaji wa sekta ya mawasiliano, teknolojia, habari na uchukuzi wa ACT Wazalendo, Ally Salehe alisema suala la TICTS kukodishwa tena au la, linapaswa kuchukuliwa kwa umakini na kufikiwa uamuzi wenye kujali na kulinda uzalendo.

“Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na TICTS, kwa kuwa ni wazi imeshindwa kukidhi matarajio ya Serikali yanayolenga kuongeza tija kwenye bandari yetu,” alisema Salehe.

Vilevile ACT wameitaka Serikali kuiwezesha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kusimamia kitengo cha makasha kwenye Bandari ya Dar es Salaam katika wakati wa mpito, huku ikiendelea na mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine mwenye uwezo zaidi.

“Serikali ifanye uchambuzi wa kina katika kutoa zabuni kwa kampuni zenye sifa ya kimataifa kupitia TICTS kwenye utendaji wake wa miaka 20 na faida zake na uwezo wa kufikisha malengo mapya ya mkataba wao,” alisema.

Pia, ACT imeitaka Serikali kuongeza usimamizi na umakini kwenye eneo hilo ili kuongeza ufanisi.

“Kwa kuwa imetajwa kuwa moja ya kilichochangia hali ya sasa kwenye bandari yetu ni kuwa Serikali haikuwekeza ipasavyo kwa yale inayowajibika nayo, ni vema jambo hilo likasimamiwa kwa umuhimu mkubwa ili kuongeza ufanisi. Bandari ni eneo muhimu sana,” alisema.

Kwa upande mwingine, ACT imeitaka Serikali kuwekeza kwenye mashirika ya umma ili kukuza uchumi kwa madhumuni ya kupata mapato, kusogeza na kutoa huduma kwa urahisi kwa jamii na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi, kudhibiti utoaji wa huduma na kulinda maslahi ya Taifa, lakini pia kutengeneza ajira zenye staha na usalama kwa wananchi wake.

“Mfumo wa sasa wa ukodishaji na uendeshaji wa sekta ya kuhudumia makasha katika Bandari ya Dar es Salaam, ni dhahiri unahatarisha uchumi wetu na haujaangaliwa kwa maslahi mapana ya Taifa,” aliongeza Saleh.


Bandari ya Dar es Salaam na mapato kwa nchi

Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato nchini, na mara kadhaa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza weledi kwenye utekelezaji wa majukumu kwa watendaji wa chombo hicho.

Hata hivyo, mara kadhaa ripoti za ukaguzi zimebaini kuwapo kwa ufanisi usioridhisha katika bandari hiyo, huku wadau wakilalamikia ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo, hivyo kuwasababishia hasara.

Kabla ya Rais Samia kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Erric Hamissi, alianza kwa kuvunja bodi ya mamlaka hiyo, huku akitoa maagizo ya kutekelezwa katika kuongeza ufanisi wa bandari. Alionekana kuchukizwa zaidi na ucheleweshaji wa mizigo na mrundikano wa makontena.

“Mkurugenzi nimekuleta hapa kusimamia bandari, Takukuru naomba, naagiza, natoa amri uchukue hatua dhidi ya watu hawa haraka sana na kama ripoti hiyo hamna nitawapatia ya nini kilichofanyika hapa. Watu waliofanya hayo wapo bado ofisini…watu tunachekeana tu, tunatazamana tu. Watu wapo maofisini wanaendeleza wizi na ubadhirifu wa mali za umma.

“Mifumo imekuwa ikichezewa, inaonyesha kuwa mizigo imelipiwa kutoka getini, lakini sio kweli haijalipiwa hivyo bandari kukosa mapato. Haya mapato yanayoonekana leo hayakupaswa kuwa hivyo yalivyo. Kama tungechukua hatua kudhibiti wizi huu tungekuwa mbali sana kwenye kukusanya mapato,” alikaririwa Rais Samia kwenye moja ya ziara zake bandari ni hapo.