ACT yataka mambo matatu kuzuia wanyama kuvamia makazi

Muktasari:

ACT- Wazalendo kimetaka kuimarishwa kwa Idara ya Wanyamapori, wananchi kupewa mbinu na uwezo wa kujihami na Serikali kufanya utafiti wa kina kubaini chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya tembo wanaoikimbia mbugani na kuvamia vijiji.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amependekeza mambo matatu ya kukabiliana changamoto ya tembo kuvamia mashamba na makazi, akisema Serikali ikiyafanyia kazi yatasaidia kupunguza kero hiyo inayowapata wananchi vijijini.

Mambo hayo ni pamoja na kuimarisha idara ya wanyamapori, wananchi kupewa mbinu na uwezo wa kujihami hasa mazao yao yanapoharibiwa na Serikali kufanya utafiti wa kina kubaini chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya tembo wanaoikimbia mbugani na kuvamia vijiji.

Ado ametoa mapendekezo hayo leo Jumatatu Oktoba 3, 2022 wakati akizungumza na wanachama wa ACT-Wazalendo pamoja na wananchi wa vijiji vya Misiaje, Malumba na Molandi vya jimbo la Tunduru Kusini wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Katika maelezo yake, Ado amesema bado kuna changamoto ya tembo kuvamia vijijini na mashamba katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya Ruvuma, Lindi, Tanga hatua inayozua hofu kwa wananchi.Hata hivyo, Ado amesema endapo Serikali itachukua mapendekezo itasaidia kupunguza tatizo hilo.

Hivi karibuni kundi la tembo wapatao 50 lilivamia mashamba na kuharibu michungwa, mikorosho na  mazao mengine katika kijiji Nkale wilayani Handeni mkoani Tanga.Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wao.


Lakini leo Jumatatu Ado amewaambia wananchi wa Tunduru kwamba, "lazima Serikali ichukue hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hii inayosumbua katika maeneo mbalimbali.Kwa kuanzia ACT tunapendekeza idara ya wanyamapori iimarishwe ili kuleta ufanisi.

"Hatua hii itasaidia kuwezesha uwepo wa askari wa kutosha wa wanyamapori kwenye maeneo yaliyoathirika na kadhia hii. Hapa Tunduru kumekuwa na matukio ya tembo kuvamia na kuharibu mashamba kwa nyakati tofauti," amesema Ado.

Kwa mujibu wa Ado, mwanzo mwaka huu, alifanya ziara katika maeneo yanayozunguka mbuga ya Selous na kukutana na changamoto kwa wananchi waliomweleza kwamba bado kuhusu tatizo la tembo kuvamia maeneo ya vijijini na mashamba na kuharibu mazao mbalimbali.

Katibu wa mkoa wa kichama wa Selous, ambaye aligombea ubunge wa Tunduru Kusini , Abdallah Mtutura amesema jimbo ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya uvamizi wa tembo kwa nyakati tofauti licha ya jitihada za  Serikali ngazi ya wilaya kulifanyia kazi.