ACT yawapitisha Shaibu, Pavu kuwania ubunge Eala

Muktasari:

  • Chama cha ACT-Wazalendo kimeungana na CUF kukamilisha mchakato wa ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) ndani ya vyama vyao, kwa kuwateua Ado Shaibu na Pavu Abdallah kukiwakilisha chama hicho kuwania nafasi za ubunge wa Eala.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, iliyoketi kwa siku mbili mfululizo imewapitisha Ado Shaibu na Pavu Abdallah kuwania nafasi ya ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala).

Kamati Kuu hiyo iliketi kuanzia Septemba 2 na 3 Jijini Dar es Salaam, ilichagua Shaibu (Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo) kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Pavu (Naibu Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu wa CT-Wazalendo) kutoka Zanzibar watakaoipeperusha bendera ya chama hicho, katika Eala.

Katibu wa Katibu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Mohammed Masaga ameiambia Mwananchi leo Jumapili Septemba 4, 2022 kwamba Shaibu na Pavu walichaguliwa jana Septemba 3, 2022 katika mchakato ulianza saa moja hadi saa tatu usiku.

“Wagombea 13 wote waliojitokeza katika kinyang’anyiro hiki walipewa dakika tatu za kujieleza kwa lugha ya Kingereza. Mchakato wa kura uliendesha hadi kuhesabiwa uliendeshwa kwa uwazi na wagombea waliishuhudia.

“Majina ya Ado na Pavu yatapelekwa katika ofisi ya katibu wa Bunge kama maelekezo yalivyotaka kwa mujibu wa mchakato huu wa Eala,” amesema Masaga.

Shaibu na Pavu wamewashinda wenzao Emmanuel Mvula, Twaha Taslima, Vincent Saguda, Mbaraka Chilumba na Samuel Sebastian, Said Chiwaya, Ester Thomas, Halima Nabalaganya,

Wengine ni Hamza Ntunu, Said Bakema, Dk Nasra Omar, Godbles Msofe, Fungo Benson, Faustine Masele na Jafet Masawe na, Godbles Msofe, Fungo Benson, Faustine Masele na Jafet Masawe.

Kwa hatua hiyo, ACT-Wazalendo imeungana na chama cha CUF, ambacho kimepeleka majina 12 katika ofisi ya katibu wa Bunge, baada ya baraza kuu la uongozi la chama hicho, kuyapitisha.

Majina yaliyopitishwa na baraza hilo ni Adui Seif Kondo,Mashaka Ngole, Mneke Said,Muhamed Ngulangwa, Queen Lugembe, Sonia Magogo, Thomas Malima, Zainab Abdul na Zainab Amir wote kutoka Tanzania Bara,

Wengine ni Mohamed Habib Mnyaa,Husna Mohamed Abdallah na Anderson Emmanuel Ndambo wote kutoka Zanzibar.

Wakati ACT-Wazalendo na CUF vikikamilisha mchakato huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaita wanachama wake 178 waliojitokeza kuchukua fomu na kurejesha ili kuwania kuteuliwa kuwania ubunge wa Eala.

Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka wagombea hao watatakiwa kwenda na nyaraka zao zote muhimu zinazohusu sifa za kuwania nafasi hizo.

Shaka amesema pamoja na mambo mengine wagombea hao wameitwa kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na uratibu wa vikao husika vya chama hicho.

Kwa upande wa Tanzania Bara, “Kikao hicho kitafanyika jijini Dodoma Septemba 4 hadi 5 mwaka huu, kuanzia saa 3 subuhi hivyo kila mwombaji anatakiwa kufika Dodoma Septemba 03 mwaka huu ili kuitika wito huo,”amesema Shaka.