Adaiwa kujiua kisa mumewe katoka jela

Muktasari:

Jesca Samson (37) mkazi wa mtaa wa Katoma, Kayanga wilayani Karagwe anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya panya baada ya kusikia mume wake aliyefungwa kutokana na ugomvi wao ameachiwa kutoka jela.

Bukoba. Jesca Samson (37) mkazi wa mtaa wa Katoma, Kayanga wilayani Karagwe anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya panya baada ya kusikia mume wake aliyefungwa kutokana na ugomvi wao ameachiwa kutoka jela.

Mwanamke huyo, kabla ya kifo chake anadaiwa pia alimnywesha sumu hiyo mtoto wake, Jordan Samson (3), ambaye hata hivyo alinusurika kifo.

Kamanda wa Polisi wa Mkao wa Kagera, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Januari Mosi saa 8:00 usiku baada ya mama huyo kutoka katika mkesha wa Mwaka Mpya.

Jesca, akiwa na ndugu zake, wakitoka kwenye mkesha, alipata taarifa kuwa mume wake ameachiwa huru na baada ya kusikia hivyo, aliwaacha njiani aliokuwa nao na kuwahi nyumbani kisha akanywa sumu hiyo.

Kamanda Malimi alisema baada ya ndugu zake kufika nyumbani, Jesca aliwaambia kuwa amekunywa sumu ya panya, ndipo walimpeleka hospitali ya Wilaya Nyakahanga pamoja na mtoto wake, na mwanamke huyo alifariki dunia Januari 2, huku mtoto wake akipona.

Mumewe ambaye hakutajwa jina, alikuwa amefungwa kifungo cha miezi mitatu jela kutokana na mgogoro wa kifamilia.

“Mgogoro uliokuwapo kati yake na mumewe ulitokana na mwanaume huyo kuuza kipande cha ardhi bila kumshirikisha mkewe na mwanamke akamshtaki katika mahakama ya mwanzo. Mume lihukumiwa kwenda jela miezi mitatu,” alisema Malimi

Alisema baada ya kusikia mme wake ameachiwa kutoka gerezani Desemba 31, 2020 alijenga hofu na hivyo kuchukua hatua za kunywa sumu ya panya na kunywesha mtoto wake.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Nyakahanga kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Malimi alilitaja tukio lingine la mauaji ambapo Amos Ludovick (39) mkazi wa Kijiji Ibale wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera anatuhumiwa kumuua mtoto wake Dastan Amos (13) kwa kipigo.

Mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Ibale.

Alisema tukio hilo lilitokea Januari 2, 2021 saa 3:00 usiku alipompiga kwa fimbo akimtuhumu kutoka nyumbani bila ruhusa ya wazazi, tangu asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.

Kamanda Malimi alisema kuwa, uchunguzi wa kitabibu umebaini chanzo cha kifo hicho ni majeraha aliyokutwa nayo mwilini ikiwa ni pamoja na kuvunjika uti wa mgongo na shingo.

Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na polisi na uchunguzi ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya mashtaka ili afikishwe mahakamani.