Adakwa na polisi akituhumiwa kusimamia kiwanda cha kutengeneza gongo
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Arusha limemkamata mwanamke mwenye umri wa miaka 31 mkazi wa Sakina kwa tuhuma za kusimamia kiwanda bubu kinachotengeneza pombe inayodhaniwa kuwa gongo.
Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha limemkamata mwanamke mwenye umri wa miaka 31 mkazi wa Sakina kwa tuhuma za kusimamia kiwanda bubu kinachotengeneza pombe inayodhaniwa kuwa gongo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema leo Jumanne Mei 25, 2021 baada ya upekuzi katika kiwanda hicho wamekamata stika 340 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na stika za usalama pakiti tatu.
Amesema kingine walichokamata ni stika 700 za pombe, vifungashio vya chupa boksi 23, chupa ndogo 483 za pombe kali, chupa kubwa 533 za pombe kali na mtambo mmoja wa kutengeneza pombe na pipa lililojaa pombe kali lita 250.
Amebainisha kuwa upelelezi unaendelea na ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
“Nitoe wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kutokomeza kabisa uhalifu katika mkoa wetu, pia nitoe onyo kuwa zoezi hili litakua endelevu na tutaendelea kuchukua hatua kali kwa watu wenye nia ya kufifisha ubora wa bidhaa za viwandani,” amesema Masejo