Afariki dunia akiacha rekodi ya kuwa na wake 39 na watoto 94

Afariki dunia akiacha rekodi ya kuwa na wake 39 na watoto 94

Muktasari:

  • Ziona Chana, mwanamume anayeaminika kuwa na familia kubwa ya wake 39 na watoto 94 amefariki dunia Juni 14, 2021, huku akicha gumzo kubwa.

Ziona Chana, mwanamume anayeaminika kuwa na familia kubwa ya wake 39 na watoto 94 amefariki dunia Juni 14, 2021, huku akicha gumzo kubwa.

Chana alifariki dunia akiwa na miaka 76, katika jimbo la Mizoram kaskazini mashariki mwa India, huku akiacha wajukuu 33 na vitukuu kadhaa. Gumzo kuhusu mwanamume huyo inatakana na jinsi alivyoweza kuhudumia familia hiyo kwa mahitaji ya kila siku ikiwamo chakula, malazi na mavazi pamoja na huduma nyingine muhimu.

Hata hivyo, alipohojiwa katika miaka ya hivi karibuni, Chana alieleza kuwa aliamini kuwa ni mtu aliyebarikiwa kuwa na familia hiyo.

Ziona Chana ni nani?

Chana alikuwa na familia yenye jumla ya watu 167 walioishi katika nyumba moja yenye ghorofa nne na wastani wa vyumba 100 katika kijiji cha Baktawng Tlangnuam.

Chana alifariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu. Chana pia alikuwa akiishi na wakwe 14 (wanawake walioolewa na watoto wake wa kiume) na wajukuu 33.

Mwanamume huyo aliyekuwa na wake 39 mpaka anafariki dunia alidai kuoa mkewe wa kwanza akiwa na miaka 17 mwaka 1959 na kuna kipindi alioa wake 10 ndani ya mwaka mmoja.

Ndoa yake ya mwisho ilikuwa mwaka 2004. Alioa wake wengi kwa kuwa dhehebu lake lilikuwa ni miongoni mwa madhehebu ya dini ya Kikristo yaliyomruhusu kuoa wake wengi.

Dhehebu hilo lilianzishwa na baba yake. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Chana alikuwa na watoto 94 waliotokana na wake hao na jumla ya wajukuu 33.

Familia hiyo iliyokuwa na watu 167 inasemekana kuwa ndiyo familia iliyokuwa na watu wengi zaidi duniani kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, japo ni kama tu utawajumuisha na wajukuu.

Hii ni kwa sababu kuna familia ya Winston Blackmore wa Canada ambayo inaaminika ndiyo yenye watu wengi zaidi kwa kuwa na watu 178.

Blackmore alikuwa na watoto 150 aliowapata kwa wake zake 27 pekee na kuifanya familia hiyo kuwa na watu wengi zaidi bila ya kujumuisha na wajukuu.

 Maisha ya familia ya Chana

Familia hiyo, iliyokuwa kivutio cha watalii pia iliishi katika kijiji cha Mizoram na ilipewa jina la ukoo wa “Chana” ambalo lilitungwa na baba wa Ziona mwaka 1942.

Katika jumba hilo kulikuwa na bweni moja kwa ajili ya wake zake wote lililopakana na chumba chake maalumu ambapo yeye alipenda kulala na wake zake saba au nane kwa wakati mmoja.

Wake zake walikuwa wakifanya zamu kulala naye, kila mmoja alikuwa akijua ratiba yake. Licha ya ukubwa wa familia hiyo alikaririwa akiiambia Reuters kwamba alitamani kuiongeza zaidi, kwani anaamini alikuwa ni mtu aliyebarikiwa Alipohojiwa miaka ya hivi karibuni, Chana alisema kwenye mlo wa jioni walikuwa wakitumia kuku 30, kilo 60 za viazi na kilo 100 za mchele kwa mlo mmoja.

Na vyakula hivyo vilipikwa kwa pamoja katika jiko moja.