Afungwa jela miaka 13 kwa kosa la kujaribu kuua

Fadina Mussa akilia kwa uchungu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara kutoa hukumu ya  kifungo cha miaka 13 jela kwa  mshatakiwa Shaibu Ally Mtepa(64)  kwa kosa la kujaribu kuua na kumjeruhi  kwa kumkata viganja vya mikono. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Mtepa afungwa jela miaka 13 kwa kosa la kujaribu kuua na kumjeruhi kwa kumkata mikono mtaliki wake Fadina Mussa, wakiwa nyumbani kwao Wilaya ya Tandahimba, awali waliishi kwa miaka 4 kama wana ndoa kabla ya mahusiano yao kukumbwa na migogoro na mfarakano na kupeana talaka.

Mtwara. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, imemhukumu Shaibu Ally Mtepa (64), kifungo cha miaka 13 jela, baada kumtia hatiani kwa kosa la kujaribu kuua na kumjeruhi aliyekuwa mke wake Fadina Mussa, kwa kumkata viganja vya mikono nyumbani kwao Tandahimba mkoani Mtwara.

Kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2023, imetolewa hukumu yake leo Julai 26 na Hakimu Mwandamizi Mwenye Mamlaka Ziada Frederick Lukuna.

Wakili upande wa utetezi Alex Msalenge amesema kuwa hayo ni maamuzi halali kwa kuwa mteja wake hakuisumbua mahakama.

“…hayo ni maamuzi halali kama mliivyosikia mteja anajutia kosa sio kwamba ameisumbua mahakama amekili kila kitu tupeni muda tuongee na mteja tutashaurina alafu tutajua hatua zinazofuata” amesema Msalenge

Kwa upande wake Fadina Mussa akilia mahakamani hapo alisema kuwa hajaridhishwa na hukumu hiyo angalau angefungwa miaka 20 ama 30 ingekuwa ni fundisho kwa watu wengine.

“Naomba Serikali inisaidie kwakuwa miaka 13 sio haki kwa mtalaka wangu ambaye ambaye aamenikata mikono yote miwili…naomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, pamoja na Rais wangu Samia Suluhu, wanisaidie,” amesema Fadina.

Kwa upande wake Clemence Mwombeki, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Door of Hope Tanzania, ambalo hufanyakazi ya utetezi, uwezeshaji na usaidizi vijana na wanawake; amesema kuwa wameipokea hukumu hiyo kama ilivyotolewa.

“Fadina Mussa alifanyiwa ukatili mkubwa sana, na hatua hii ni ya mahakama ni ya kupongezwa. Kiufupi Tayari mahakama imemtia hatiani mtenda kosa, na imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 13 jela. Ni matukio machache yanayofikia hatua hii,” amesema Mwombeki na kuongeza;

“Ukilinganisha na matukio yanayotokea mkoani Mtwara, hatua hii ni kubwa sana. Kuna matukio mengi ya ukatili ambayo hutokea ndani ya ya Mkoa wa Mtwara, kwa mwaka jana tu; kuna zaidi ya matukio 172 ya ukatili yakiwahusisha wananwe na watoto.”

Hivyo basi, Mwombeki amesema: “Kwa kuwa mhanga hajaridhika na hukumu, tutamshauri ni nini cha kufanya, maana tendo alilotendewa, limemuacha na ulemavu wa kudumu, na kumbuka yeye ndiyo alikuwa akiisaidia familia yake.”