AG amfikisha Madeleka kwa Kamati ya Maadili ya Mawakili

Muktasari:
Madeleka amesema anafanya mchakato wa kusambaza nakala kwa mawakili watakaosimama kumtetea.
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi amewasilisha malalamiko kwa Kamati ya Maadili ya Mawakili dhidi ya wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka.
Anamlalamikia kwa kukiuka maadili ya kitaaluma.
Barua ya wito wa Madeleka mbele ya kamati hiyo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii leo Februari 23, 2024 ikieleza AG amewasilisha malalamiko dhidi ya wakili huyo kuhusu ukiukaji wa maadili ya kitaalumu.
Kilichomo kwenye wito
Barua ya wito wa Madeleka mbele ya kamati hiyo ya mawakili, imebeba ujumbe unaosema, “tuhuma za kuvunja miiko ya kitaaluma kutoka kwa AG.”
Barua hiyo ya Februari 20, 2024 ambayo Madeleka ameipokea Februari 23, 2024 imetiwa saini na Katibu wa kamati, Faraji Ngukah.
Imesema kamati imepokea malalamiko dhidi ya Madeleka kutoka kwa AG.
“Unatakiwa kisheria ujibu madai yaliyoibuliwa katika hati ya kiapo, nakala yake imeambatanishwa. Majibu yako yanapaswa kufika ndani ya siku 21 kutoka siku uliyopokea wito,” imeeleza barua hiyo.
Kulingana na barua hiyo, iwapo hatazingatia ndani ya muda uliopangwa, kamati itaendelea bila kutoa taarifa nyingine zaidi.
Si Madeleka pekee
Mbali ya Madeleka, mawakili wengine waliokwisha kulalamikiwa mbele ya kamati hiyo ni Boniface Mwabukusi.
Aliitwa mbele ya kamati Oktoba 2023 akilalamikiwa kwa utovu wa nidhamu. Malalamiko yaliwasilishwa na Dk Feleshi.
Mwaka 2018, Fatma Karume alikumbana na kadhia hiyo, aliposhitakiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Profesa Adelardus Kilangi. Shauri dhidi yake lilienda mbali zaidi hadi kusimamishwa kutoa huduma za uwakili.
Alichosema Feleshi
Alipotafutwa na Mwananchi leo Februari 23, 2024 kuzungumzia malalamiko dhidi ya Madeleka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi amesema ni mapema mno kuizungumzia.
Amemshauri mwandishi wa habari kusubiri siku iliyotajwa ili wakasikilize au kupewa taarifa.
“Huu ndiyo kwanza wito, unaandikaje habari kutokana na wito. Mnapaswa msubiri siku iliyopangwa kwa ajili ya kesi kusikilizwa kama kuna nafasi ya ninyi kuingia mtaingia kusikiliza au kama sivyo mtapewa taarifa na mamlaka sahihi,” amesema.
Alichosema Madeleka
Akizungumza na Mwananchi kuhusu hilo leo Februari 23, Madeleka amekiri kupokea wito huo, akifafanua si barua pekee bali ilihusisha na nyaraka nyingine za kesi aliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Madeleka anadai anashitakiwa kutokana na kuhusika kwake katika kesi ya Hashim Ally dhidi ya mbunge wa Babati, Pauline Gekul.
Baada ya kupokea barua ya wito wa kufika mbele ya kamati na nyaraka za shauri hilo, Madeleka amesema anafanya mchakato wa kusambaza nakala kwa mawakili watakaosimama kumtetea.
“Kwa sasa nafanya mchakato wa kutoa nakala ili nisambaze nyaraka hizi kwa mawakili watakaosimama kunitetea, lakini hata kwa Watanzania na wapenda haki,” amesema Madeleka.
Kwa mtazamo wa kisheria, Madeleka anadai kilichofanyika dhidi yake ni kinyume cha utaratibu, kwani AG hana mamlaka ya kumshitaki katika kamati hiyo.
Mamlaka ya AG yanakosekana kutokana na kile alichodai kiongozi huyo ni sehemu ya kamati ya maadili ya mawakili, hivyo haiwezekani akawa mlalamikaji kwenye kesi inayohukumiwa naye.
“Kanuni za haki za asili zinasema mtu hawezi kuwa hakimu kwenye kesi yake mwenyewe. Kwa vyovyote atajipendelea,” alidai Madeleka.
Lakini kisheria si lazima AG kuwa sehemu ya wajumbe wa kamati hiyo, wapo watu wanaoweza kuwemo badala yake kama inavyofafanua, Ibara ya 4, 1(b) ya Sheria ya Mawakili.
Kulingana na ibara hiyo, wanaohusika katika kamati hiyo pamoja na wajumbe wengine ni AG au Naibu wake au Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP).
“Kamati hiyo itamhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) au Naibu wake au Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP),” inaeleza ibara hiyo.