Aga Khan Tanzania yaziwezesha hospitali sita

Muktasari:

Taasisi ya Utoaji huduma za Afya Aga Khan, Tanzania (AKHA, T) imezindua jukwaa la mafunzo ya kidigitali kwa watoa huduma wa afya juu ya matibabu ya wagonjwa wenye changamoti kubwa wakiwemo wale waliothiriwa na maambukizi ya Uviko - 19 wanaohitaji matibabu ya wagonjwa mahututi.

Dar es Salaam. Hospitali sita za Serikali ndani ya Jiji la Dar es Salaam zimekabidhiwa vifaa na zana za teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka Taasisi ya Utoaji huduma za afya Aga Khan Tanzania (AKHS,T).

 Ni katika uzinduzi wa jukwaa la mafunzo ya kidigitali kwa watoa huduma za afya.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wataalamu juu ya matibabu ya wagonjwa wenye changamoto kubwa wakiwemo walioathiwa na maambukizi ya ugonjwa virusi vya Korona (Uviko-19) wanaohitaji matibabu ya wagonjwa mahututi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Meneja Programu wa Taasisi ya utoaji huduma za Afya Aga Khan, Theresia Mohere amesema jukwaa hilo ni sehemu ya shughuli zinazotekelezwa kupitia mradi wa ubia wa kukabiliana na Uviko-19, Afrika Mashariki uliofadhiliwa na umoja wa Ulaya.

"Mradi huu unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na Uviko-19 kwa kuimarisha mifumo ya afya na utoaji wa huduma," amesema Mohere.

Mradi huo wa miaka miwili na nusu ambao unatajwa kuleta matokeo makubwa katika sekta ya afya, unatarajia kuwafikia watu 700,000 pindi utakapokamilika na kuunda mfumo fanisi wa utoaji huduma za afya na udhibiti wa Uviko-19.

Kupitia vifaa hivyo, watoa huduma wataweza kupata nafasi ya kujifunza vitu mbalimbali vinavyohusiana na Uviko-19 ili waweze kuongeza ufanisi katika huduma wanazotoa.

Hospitali zilizopewa vifaa hivyo vilivyo na thamani ya Sh20 milioni ni Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Hospitali ya mkoa ya Rufaa Amana, Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Hospitali ya Sinza na Mbagala.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume amesema anatambua thamani ya kujitoa kwa wabia wote wanaohusika kuandaa na kutekeleza mradi huo.

"Tunaishukuru timu ya usimamizi wa vituo vyote, washirika kwa uongozi na usaidizi wenu wakati wa hatua ya utekelezaji. Nahimiza taasisi washirika kuendelea kubuni miradi endelevu ya afya jijiji Dar es Salaaam na nchi nzima iki kuleta matokeo zaidi kwa wahitaji," amesema

"Pia Umoja wa Ulaya na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan na Taasisi zake tunawashukuru kwani wanajitahidi sana kushughulikia maeneo mahsusi yenye uhitaji mkubwa na kuweka mifumo inayosaidia vituo vya ubia kwa kuwezesha uunganishaji wa teknolojia ya habari na huduma ta afya ambayo hivi leo inagusa watu wengi," amesema Dk Mfaume.