Agizo la JPM lazuia makontena 262 ya mchanga

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuweka lakiri maalumu za utambuzi katika moja ya makontena 262 yenye mchanga wa madini jijini Dar es Salaam jana. Picha na mpiga picha wetu.

Muktasari:

Makontena hayo yamezuiwa ikiwa ni siku mbili baada ya Rais Magufuli kushuhudia makontena 20 katika bandari hiyo yakiwa na mchanga wenye dhahabu.

Baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye dhahabu kwenda nje ya nchi, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imezuia makontena 262 yenye mchanga huo uliokuwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Makontena hayo yamezuiwa ikiwa ni siku mbili baada ya Rais Magufuli kushuhudia makontena 20 katika bandari hiyo yakiwa na mchanga wenye dhahabu.

Baada ya kuyashuhudia, Rais Magufuli aliagiza makontena hayo kutosafirishwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Rais alitoa zuio hilo ikiwa ni mara ya pili alipotembelea kiwanda cha vigae cha GoodWill wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani kinachotumia teknolojia ya kuchemsha baadhi ya malighafi na kuchambua madini yanayotakiwa kwa ajili ya utengenezaji wa vigae na marumaru.

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema baada ya Rais Magufuli kushuhudia makontena bandarini Alhamisi iliyopita, uongozi ulianzisha operesheni ya ukaguzi ili kubaini kama kuna mchanga wa dhahabu. “Baada ya operesheni tumebaini makontena 262 yenye mchanga wa dhahabu ambayo yalikuwa tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi,” alisema.

Kakoko alisema makontena hayo ni mali ya mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia na yalikuwa yamehifadhiwa katika Bandari Kavu ya Mofed iliyopo Kurasini wilayani Temeke.

Kakoko alisema makontena hayo ambayo yalikuwa na lakiri (seal) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA, yalikuwa yakisafirishwa na Wakala wa Forodha ya Freight Forwarders Tanzania Limited iliyopo Dar es Salaam.

“Makontena yenyewe yalikuwa katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kiforodha kusafirisha mzigo huo,” alisema.

Alisema makontena hayo yalipokewa katika bandari hiyo kati ya Desemba 17, 2016 na Machi 4, 2017 yakitokea katika migodi ya Buzwagi na Pangea.

Kakoko alisema hata kama mchakato wa kusafirisha makontena hayo ulianza kabla ya katazo la Rais, wahusika walitakiwa kutoa taarifa za kuwa na nzigo wa aina hiyo bandarini. “Katazo la Rais ni sheria hatuwezi kuuacha mzigo huo usafirishwe kwenda nje ya nchi wakati tayari Rais amepiga marufuku,” alisema na kuongeza:

“TPA itahakikisha inashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti usafirishaji holela wa rasilimali za nchi,” alisema.

Pia, aliuomba uongozi wa TRA kuwaondoa wafanyakazi wasiokuwa waaminifu ambao walishiriki kuusafirisha mzigo huo.

Aliitaka Kampuni ya Upakujaji na Upakiaji wa Makontena Bandarini (Ticts) kutoa ushirikiano katika usalama wa mizigo inayotoka na kuingia bandarini.

Kakoko alisema wataendelea kusaka makontena kwenye bandari kavu ili kubaini kama kuna rasilimali za nchi ambazo haziruhusiwi kusafirishwa nje ya nchi.

“Kiusalama bandari yetu ni miongoni mwa bandari zinazoongoza kwa usalama,” alisema.

Akizungumzia hilo, Kamanda wa Polisi wa Bandari ya Dar es Salaam, Ramadhani Mvungi alisema sasa bandari hiyo ina ulinzi mkali kutokana na kuwapo kwa vifaa vya kisasa vya ukaguzi.

“Hakuna tone la mchanga litakalopita kwenda nje ya nchi baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku, tuko imara kulinda rasilimali za nchi,” alisema.

Mfanyakazi wa Bandari Kavu ya Mofed, Godfrey Peter alisema bosi wake anauguliwa na mtoto, hivyo alishindwa kutoa taarifa mapema za kuwepo kwa mchanga huo. “Ni kweli mchakato wa usafirishaji wa mchanga huu ulianza kabla ya agizo la Rais, lakini uongozi ulichelewa kutoa taarifa kwa sababu za kuuguliwa,” alisema.

TRA wazungumza

Akizungumzia kuhusu makontena hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema katika suala la kutoa huduma ya uendeshaji kuna hatua mbalimbali, hivyo inawezekana ziliwekwa hizo lakiri kabla ya kutolewa agizo la kuzuia.

“Cha muhimu ninachokiona na ni cha faida kwa nchi ni mchanga kuzuiwa, hayo mambo mengine ya utendaji yanahitaji muda kuyafafanua hayawezi kueleweka kwa urahisi hadi uwe eneo la tukio na uone ni nini na taratibu zake zilifanyika lini,” alisema.

Acacia wazungumza

Akizungumzia makontena hayo, Meneja wa Uhusiano na Serikali wa Kampuni ya ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Asa Mwaipopo alisema makontena hayo ya makinia ya shaba (mchanga wa madini) yalifikishwa bandarini hapo kabla ya zuio la Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Acacia, kila mwaka migodi hiyo husafirisha wastani wa tani 55,000 za mchanga huo unaojumuisha madini ya dhahabu, shaba, chuma, salfa na mercury.

“Huo mzigo ulikuwa upo njiani kutoka Buzwagi na Bulyanhulu na mwingine tayari ulishafika bandarini. Makontena yote yalishalipiwa kodi TRA, piga hesabu kodi asilimia nne ya Dola 100,000 (za Marekani) kutoka kila kontena, leseni ya kusafirishia tulikuwa tumeshapewa na Wizara ya Nishati na ukaguzi ulishafanywa na TMAA (Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania),” alisema.

Mwaipopo alisema kwa sasa bado wanaendelea na mazungumzo na Wizara ya Nishati na Madini kuishawishi kuendelea na usafirishaji wa mchanga huo kwa kuwa Tanzania hakuna mtambo wa kuchenjua madini hayo.

Meneja huyo alisema mgodi wa Buzwagi unazalisha gramu mbili za dhahabu katika tani moja ya mchanga, lakini unapopelekwa kuchenjuliwa huwa wanapata wastani wa gramu 120 hadi 150 katika kila kontena. Thamani ya kila kontena ni Dola100,000 za Marekani hadi 150,000.

Kwa mujibu wa hesabu hiyo, makontena hayo 262 yatakuwa na thamani inayofikia wastani wa Sh69.1 bilioni (kwa wastani wa Dola120,000 za Marekani kila kontena).

Mwaipopo alisema kila siku mgodi wa Buzwagi unazalisha kati ya makontena manne hadi matano ya mchanga huo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCEM), Gerald Mtuli aliliambia gazeti hili kuwa upembuzi yakinifu uliofanyika mwanzoni wakati wa uwekezaji wa migodi hiyo ulionyesha migodi hiyo itahitaji kusafirisha mchanga huo kwa kuwa inategemea wastani wa asilimia 30 ya mapato kupitia mchanga huo.

Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Kelvin Matandiko na Kalunde Jamal.