Agizo la Rais Samia lachukua sura mpya walioongeza fedha ununuzi wa ndege

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akizungumza bungeni. Picha na mtandao

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema mifumo ya malipo ipo imara, huku akidai waliohusika kuongeza fedha za manunuzi ya ndege hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatano April 6, 2023  wakati akimpa taarifa Mbunge wa Viti Maalum, Ester Matiko alipokuwa akichangia  bungeni  mjadala wa  makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha  2023-2024.

Katika mchango wake Matiko amedai kuna ubadhilifu mkubwa katika ununuzi wa ndege huku wahusika wakikaa kimya bila kusema jambo lolote.

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alionesha kuchukizwa na kitendo cha ongezeko la fedha za manunuzi ya ndege mpya ya mizigo kinyume na fedha ambazo zilizokuwa kwenye mkataba wa awali akataka Watumishi wa Serikali waliokubali ongezeko hilo bila kuhoji waachie nafasi zao kwakuwa hawana uchungu na fedha za Watanzania.

“Kuna mradi hapa tumetengeneza ndege ya mizigo ambayo tunakaribia kuipokea, last Installments ilikuwa tulipe Dola Milioni 37, invoice imekuja Dola milioni 86….. unauliza mkataba ulisemaje? hii imetokana na wapi?, ooh vifaa vimepanda bei, vipi? mkataba wetu ulisemaje,” alinukuliwa.

Matiko amesema haikubaliki na haiingia akilini kwani litakuwa Taifa la ajabu kuruhusu watendaji hao kuendelea kukaa huku akimtupia kijembe Waziri wa Fedha kwamba kila siku anavaa tai ya Tanzania inaoonyesha uzalendo lakini akahoji uko wapi uzalendo huo.

Katika taarifa yake Dk Mwigulu amesema utaratibu wa malipo uliowekwa hapa nchini ni imara hauna vitu  vya hovyo hovyo vinaweza kupita.

Amesema hakuna malipo ya kila mwezi yanayoenda kufanyika bila Rais kujua na mahitaji yote yalikienda Wizara ya Fedha na Mipango wanaombea ridhaa kwa Rais.

“Na hata hilo la ndege unalolisema yalipoletwa mahitaji Wizara ya Fedha tuliliona lina ongezeko ambalo kama ni la kimkataba lazima tupate ushauri wa Mwanasheria Mkuu,” amesema Waziri Mwigulu.

Alipoulizwa na Spika kama anaipokea taarifa hiyo, Matiku alisema : “Mheshimiwa Spika nitakuwa sijitendei haki, siipokei.

Akiendelea kuchangia mbunge huyo amehoji malipo hayo ni makubwa Je yale madogo ambayo yamekuwa yakifanywa na watendaji wa Serikali inakuwaje.