Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahadi za Marekani kwa Russia majanga

Rais wa Russia, Vladimir Putin akiwa na Rais wa zamani wa Marekani, George W Bush kwenye moja ya ziara zao. Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Swali lililobaki kiporo katika toleo lililopita ni je, upanuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (NATO) ulikuwa “kosa baya zaidi la sera ya Marekani katika enzi ya baada ya Vita Baridi kama George Kennan alivyodai?

Miongoni mwa wabunifu wa NATO walibadilisha mawazo yao kuhusu Russia baada ya kuporomoka kwa Shirikisho la Urusi, wakahimiza kuwa uwepo utaratibu wa usalama wa Ulaya, wakionya kwamba kutengwa kwa Russia kungekuwa na matokeo yasiyotarajiwa, na ya hatari.

Mwaka 1992, Muungano wa Kijeshi ya Umoja wa nchi za Kikomunisti uliojulikana kama Mkataba wa Warsaw ulikuwa unatoweka kwa kishindo, na utawala wa George H. W. Bush wa Marekani ulikabiliwa na Russia iliyodhoofika sana kwa kubomoka vipande vipande na iliyoacha ombwe la usalama katika Ulaya ya Kati na Mashariki.

Katika kukabiliana na hali hiyo, suluhu ambayo utawala wa Bush uliona inafaa ni kuunda Baraza la Ushirikiano la Atlantiki ya Kaskazini (North Atlantic Cooperation Council—NACC).

Baraza hilo lilikutana kati ya mwaka 1991 na 1997 na kujadili masuala yaliyohusiana na uondoaji wa wanajeshi wa Russia, lakini lilikuwa na wanachama wengi na ajenda tofauti.

Mwaka 1997, baraza hilo likabadilika na kuwa Baraza la Ushirikiano wa Euro-Atlantic (EAPC) na likawa na wanachama 50.

Baraza hili lilikuwa suluhu ya muda kwa tatizo lenye changamoto nyingi zaidi. Wakajikuta wanakabiliwa na swali moja la msingi. Je, wanaweza kuunda chombo kipya cha usalama ambapo Russia na Ulaya Mashariki zingekuwa na jukumu la kutekeleza?

Nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki, ambazo zilikuwa zimekombolewa upya kutoka kwenye udhibiti wa Shirikisho la Urusi na zikikabiliwa na matatizo ya kisiasa ya ndani na ya kiuchumi, zilikuwa zimeanza kufikiria changamoto za usalama ambazo zingekabiliana nazo katika ulimwengu mpya wa baada ya Russia.

Wakati huo huo, Russia ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa zaidi, huku ikizidi kupoteza milki yake kwa sababu ya nchi nyingi kujitenga nayo.

Russia yenyewe iliibuka mwaka 1992 ikiwa na eneo dogo kuliko ilivyokuwa karne nne kabla, tena bila eneo la ulinzi. Russia ilikuwa imepoteza majimbo ambayo Kremlin iliamini ni muhimu kwa usalama wa Serikali.

Kwa kurejea nyuma, Marekani na washirika wake walidharau sana kuanguka kwa Shirikisho la Urusi.

Russia iliona usalama wake unatiwa hatarini, hususan ikizingatia ukosefu wa usalama na wasiwasi katika nchi za Ulaya ya Kati.

Vyombo kadhaa vya kujihami na kuilinda Ulaya kama vile NATO, pamoja na kwamba vilipunguza hofu ya usalama ya nchi za Ulaya ya Kati, vilizidisha wasiwasi nchini Russia, na kwa sababu hiyo kupanuka kwa NATO kukawa ni suala muhimu kwa usalama wa Russia. NATO iliongeza kujiamini kwa Marekani na washirika wake, lakini ikapunguza kujiamini kwa Russia.

Mwaka 1993, kitengo cha Ujasusi ya Kigeni wa Russia, wakati huo kikiongozwa na mwanadiplomasia mkongwe Yevgeny Primakov, kilionya dhidi ya upanuzi wa NATO na kuweka bayana ni nini ungekuwa msimamo wa Russia.

“Upanuzi huu,” Primakov alisema, “utaleta kundi kubwa zaidi la kijeshi ulimwenguni pamoja na uwezo wake mkubwa wa kuleta kero za moja kwa moja kwenye mipaka ya Russia ... Hili likitokea, tutalazimika kuhitaji ulinzi kwa upande wetu, kupeleka tena vikosi vya jeshi na kubadilisha mbinu zetu za kujiendesha.” Kisha akasisitiza, “Russia ina haki ya maoni yake kutiliwa maanani.”

Labda muhimu zaidi kuliko kile ambacho aliyekuwa Rais wa Urusi, Mikhail Gorbachev, aliambiwa au hakuambiwa mwaka 1990 kuhusu NATO ni kile alichoambiwa Boris Yeltsin mwaka 1993.

Oktoba 1993, muda mfupi baada ya Yeltsin kutumia mabavu kusambaratisha makundi ya wapinzani katika bunge la Urusi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Warren Christopher alizuru Moscow kuelezea wazo la ‘Ushirikiano wa Amani’.

Utawala wa Rais Bill Clinton wa Marekani na washirika wake walipoanza kujadiliana jinsi ya kupanga upya usalama katika Bara la Ulaya katika miaka ya 1990 kwa namna ambayo ingeipa Russia nafasi, haukuacha nia yake ya kuendelea NATO ambayo Russia walitaka isiwepo.

Ingawa Warusi wengi na baadhi ya nchi za Magharibi walipaza sauti za kutaka kuifutilia mbali NATO ambayo kwao waliiona kama ni masalia ya Vita Baridi na badala yake kuweka shirika la Umoja wa Ulaya ambalo lingeijumuisha Russia, Marekani na Ubelgiji, wengine hawakuona sababu ya kuvunja muungano huo ambao, kwa maoni yao ni umoja uliofanikiwa sana.

Badala yake NATO iliamua kuunda Ushirikiano wa Amani (PfP—Partnership for Peace). Mpango huu wa PfP uliruhusu nchi yoyote kujenga uhusiano wa kibinafsi na NATO na kuchagua vipaumbele vyao wenyewe kwa uhusiano huo. Kwa hiyo Russia nayo ingeweza kutumia mpango huo kujenga uhusiano na nchi yoyote mwanachama wa NATO.

Kwa maana hii, kila nchi ingetengeneza programu yake na nchi nyingine chini ya PfP, na kwa wengine ingekuwa ni hatua ya kwanza kuelekea kuwa mwanachama wa NATO. Baadhi ya maafisa wa Marekani walikusudia PfP iwe mbadala wa uanachama wa NATO, lakini kwa nchi nyingine hawakukubaliana na hilo.

Wakati Waziri Christopher alipomweleza Rais Yeltsin kwamba hakuna kitakachofanywa kwa lengo la kuitenga Russia katika “kushiriki kikamilifu usalama wa Ulaya katika siku zijazo,” Yeltsin aliidhinisha Russia kuingia kwenye mpango wa PfP.

Lakini, Yeltsin akamwomba Christopher aahidi kwamba PfP ilimaanisha ushirikiano, na si uanachama, kwa mataifa ya Ulaya ya Kati yaliyoshiriki katika hiyo PfP. Waziri Christopher alimhakikishia kwamba ndivyo ilivyo.

“Hili ni wazo zuri, ni wazo la fikra,” Yeltsin alijibu. Hiyo ni kwa mujibu wa kitabu ‘Before and After the Fall: World Politics and the End of the Cold War’ kilichoandikwa na Nuno P. Monteiro, Fritz Bartel.

Baadaye, Christopher alisema Marekani itakuwa “ikiliangalia suala la uanachama kama tukio la muda mrefu,” lakini haijulikani jinsi Yeltsin alivyoitikia hilo. Kwa mujibu wa mwandishi M. E. Sarotte katika kitabu chake, ‘Not One Inch: America, Russia, and the Making of Post-Cold War Stalemate’, Rais Yeltsin “alilegea”.

Hatimaye Jumatano ya Juni 22, 1994, ambayo ilikuwa ni siku ya kuadhimisha miaka 50 ya uvamizi wa Adolf Hitler, Russia ilitia saini makubaliano yake ya PfP.

Lakini, wengine huko Moscow walikuwa na shaka zaidi juu ya PfP. Walisema dosari yake kubwa ni kuwa haikutambua hadhi maalumu ya Russia kama taifa lenye nguvu.

Waziri wa Ulinzi wa Russia, Pavel Grachev alitangaza kuwa ikiwa Russia itajiunga na PfP, inapaswa kuwa na jukumu maalumu na uhusiano maalumu na NATO. Lakini Marekani ikamjibu kuwa mpango wa aina hiyo “haupo” na kwamba Russia ingetia saini makubaliano yake ya PfP kwa msingi uleule unaotumiwa na nchi nyingine yoyote.

Mabalozi wawili wa Marekani—James Collins na Thomas Pickering—baadaye walikiri kwamba Marekani ilipuuza ahadi zake kwa kukubali nchi za Ulaya ya Kati kujiunga na NATO wakati wa utawala wa Clinton.

Kwa maana hii, Yeltsin alikuwa sahihi kwa kuamini kwamba ahadi za wazi zilizotolewa mwaka 1993 kuhusu NATO kutojipanua huko Ulaya ya Kati kwa siku zijazo zilivunjwa wakati utawala wa Clinton ulipoamua kutoa uanachama kwa Ulaya ya Kati.

Je, nini kilifuata baada ya hapo? Tukutane kesho.