Ahueni yazidi kuonekana bei ya mafuta

Muktasari:

Taarifa ya Ewura imeonyesha kuwa kuanzia Jumatano Novemba 2, mkoani Dar es Salaam bei ya petroli itabaki kama ilivyo Sh2, 886 kwa lita moja na dizeli imeshuka kidogo kwa Sh31 kutoka Sh3, 083, huku bei ya mafuta ya taa ikipungua kwa Sh224 na kufikia Sh3, 11.

Dar es Saalam. Ahueni za bei ya mafuta imezidi kuonekana kwa miezi mitatu mfululizo huku hali hii ikiakisi kushuka kwa bei za soko la mafuta la dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Jumanne Novemba 1, 2022 imeonyesha kuwa kuanzia kesho Jumatano mkoani Dar es Salaam bei ya petroli itabaki kama ilivyo Sh2, 886 kwa lita moja na dizeli imeshuka kidogo kwa Sh31 kutoka Sh3, 083 hadi Sh3, 082, huku bei ya mafuta ya taa ikipungua kwa Sh224 na kufikia Sh3,111.



Hata hivyo, taarifa ya wa mtandao wa ‘Trending Economics’ inaonyesha hadi Novemba 2022, bei ya mafuta ghafi kwa pipa ilikuwa ikiuzwa kwa Dola 88.56 za Marekani sawa na Sh203,688 ikiwa imeongezeka kwa Sh1,518 ikilinganishwa na bei ya Oktoba.

Bei ya mafuta ghafi imekuwa ikipungua kutoka Dola 103.6 (wastani wa Sh238,280) , kwa Julai hadi kufikia Dola 94.9 (wastani wa Sh218,270), Dola 90.4 ( wastani wa Sh207,920) Septemba na 87.9 Oktoba (wastani wa Sh202,170).

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Serikali imeendelea kutoa ruzuku kwenye bidhaa hizo ikilenga kupunguza ukali wa bei.

Serikali ilitoa ruzuku ya Sh59.58 bilioni kwa ajili ya bei za mafuta ya Oktoba 2022, ikiwa ni kiwango kidogo zaidi ukilinganisha na Sh65 bilioni iliyotolewa mwezi Septemba huku mwezi huu haijataja kiasi cha ruzuku iliyotolewa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, Mkoa wa Tanga bei ya mafuta ya petroli imeshuka kutoka Sh2, 924 Oktoba hadi Sh2, 806 mwezi huu huku dizeli ikipungua kwa Sh34 na kuwa Sh3, 074, Mtwara bei ya petroli imepanda kutoka Sh2, 908 Oktoba hadi Sh2, 917 mwezi huu.