AI sasa kuingizwa kwenye mfumo wa elimu nchini

Makamu mkuu wa Chuo kikuu Cha Dodoma,profesa Lughano Kusiluka akizungumza walivyojipanga na Akili Bandia

Muktasari:

  • Kuingizwa kwa mfumo huo ni utekelezwaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusisha mitaala elimu kuona umuhimu wa kuingiza mambo ambayo yanakwenda na Technolojia za kisasa.

Arusha. Wizara ya Elimu, Sayansi na Technolojia, imekamisha sera ya matumizi ya ‘Akili Bandia’ (AI) katika mifumo ya elimu nchini.

Kuingizwa kwa mfumo huo ni utekelezwaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusisha mitaala elimu kuona umuhimu wa kuingiza mambo ambayo yanakwenda na teknolojia ya za kisasa.

Naibu  Waziri wa Elimu, Sayansi na Technolojia, Omary Juma Kipanga  ametoa taarifa hiyo Leo Novemba 15,2023 wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wanasayansi barani Afrika, ambao unajadili juu ya utayari wamatumizi ya AI kwa mtazamo wa kiafrika katika kuelekea mapinduzi ya viwanda, kukuza uchumi na tafiti.

Amesema AI kwa sasa itaingizwa katika mitaala ya masomo ya Tehama ili kuwaandaa wanafunzi kuweza kuitumia teknolojia hiyo katika masomo yao lakini pia kuwezesha kufanya bunifu mbalimbali.

"Mitaala yetu itaingiza Akili Bandia kuanzia shule za msingi hadi vyuoni ili kupata wanafunzi ambao watabobea katika teknolojia," amesema.

Makamu Mkuu wa Chuo Cha Sayansi na Technolojia cha Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula amesema matumizi ya AI yatasaidia sana kuboresha uzalishaji wa nafaka, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu

"Hivyo lengo la mkutano huu wa leo ni kuwakutanisha wanasayansi kujadiliana maendeleo ya tafiti kwa kutumia AI," amesema

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lughano Kusiluka amesema AI ina faida na hasara japo kidogo.

Profesa Kusiluka amesema watanzania hawana sababu ya kuogopa akili hizo bandia akidai kuwa in manufaa makubwa na kwamba tayari vyuo vikuu vimeanza kutoa elimu ya ubunifu kuhusiana na teknolojia hiyo.

Amesema vyuo vikuu tayari vimejipanga kudhibiti wanachuo wavivu ambao watataka kutumia AI kujibu mitihani na kufanya maandiko mbalimbali.

Amesema Akili bandia inasaidia sana kujifunza lakini ni muhimu kuchanganya ya elimu ya kibinaadamu.

Mkutano huo wa kimataifa unashirikisha zaidi ya nchi 25 na umedhaminiwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwepo SIDA, IDRC-CRDI, IEEE na kuandaliwa na vyuo vikuu vya Dodoma na Nelson Mandela.