Ajali nyingine Morogoro, lori laacha njia na kuua watatu

Muktasari:

  • Watu watatu wamefariki na mmoja kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa likitokea mkoani Ruvuma kuelekea Jijini Dar es salaam kuacha njia na kugonga gari na mtembea kwa miguu na nyumba iliyopo kando ya barabara kuu ya Morogoro-Iringa.

  

Morogoro. Watu watatu wamefariki na mmoja kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa likitokea mkoani Ruvuma kuelekea Jijini Dar es salaam kuacha njia na kugonga gari na mtembea kwa miguu na nyumba iliyopo kando ya barabara kuu ya Morogoro-Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 25, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim amesema ajali hiyo imetokea saa 1.30 asubuhi katika eneo la Kidoma wilayani Kilosa, baada ya lori aina ya Faw iliokuwa na tela Mtoto kushindwa kusimama kwenye mzunguko (round About) na hivyo kuhama kutoka upande wake kwenda upande mwingine.

Kamanda Muslim amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori hilo aliyetambulika kwa jina la Hamadi Awadhi (38) mkazi wa Tanga kushindwa kulidhibiti na hivyo kugonga gari lililokuwa limepaki upande wa kulia Katika kivuko cha watembea kwa miguu aina ya Faw lilikuwa likiendeshwa na Victor Fili (49) Raia wa Zambia ambaye alikuwa akitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Nchini Zambia.

Amewataja watu waliogongwa na gari hilo kuwa ni pamoja na Rehema Ramadhani (45) mkazi wa Mikumi kabla ya gari hilo kuvamia nyumba ya Joakim Kimaro (78) mkazi wa Mikumi  na kusababisha majeruhi 4.

Amesema majeruhi watatu walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi, akiwemo dereva wa lori lililosababisha ajali (Hamad Awadhi) na utingo wake ambaye hakufahanika jina pamoja na Rehema Ramadhani mtembea kwa miguu.

Amemtaja majeruhi mmoja kati ya wanne kuwa ni Selemani Kapoma (27) ambaye alikuwa abiria Katika lori hilo na amelazwa Katika hospitali ya Mtakatifu Kizito akipatiwa Matibabu.

Akizungumza na Mwananchi, daktari wa zamu katika hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Kizito, Iliyopo Mikumi, Simon Nkwela, amekiri waliopokea majeruhi  wanne, ambapo watatu ni wanaume na mwanamke mmoja  aliyekuwa akilalamikia maumivu makali ya tumbo.

Hata hivyo, daktari huyo amesema wakati wanafanya maandalizi ya vifaa ili kumfanyia upasuaji tumbo lake liliendelea kuvimba akafariki dunia pamoja na wengine wawili wanaume.

Pia amesema majeruhi aliyelazwa hospitalini hapo ameumia zaidi sehemu ya jicho na kwamba anaendelea na matibabu hospitalini hapo.