Ajali yaua mtu mmoja Kilimanjaro
Muktasari:
- Mtu mmoja amefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa katika eneo la Kisangara Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro baada ya dereva wa Hiace kupoteza mwelekeo na kwenda kugonga lori la mizigo.
Mwanga. Mtu mmoja amefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa katika eneo la Kisangara Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya dereva wa Hiace kupoteza mwelekeo na kwenda kugonga lori la mizigo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanajro, Ronald Makona amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Jumapili Julai 18 ambapo amesema ajali hiyo imetokea eneo la Kisangara kata ya Lembeni katika barabara kuu ya Mwanga-Moshi.
Kamanda Makona amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Emmanuel Mkuli (32) ambaye ni dereva Hiace kuligonga gari aina ya SAU lililokuwa likiendeshwa na dereva Mnyaruwanda, Mazimbaka Teoniste akitokea Mwanga kuelekea Same.
Aidha amewataja majeruhi kuwa ni, William Hassan(32), Asha Hussein (65) na Imani Othman (18) ambao wote wamekimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC kwa ajili ya matibabu.
"Chanzo cha ajali hii ni dereva wa Hiace kwenda kulia zaidi mwa barabara na kugongana na lori lililokuwa likitokea Wilaya ya Mwanga kwenda Same,"amesema Kamanda Makona
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same.