Prime
Ajifungua pacha wanne, mmoja afariki
Daktari, Amos Katisho akimuhudumia Fatuma Idd (26) aliyejifungua watoto wanne katika Kituo cha Afya cha Filbert Bayi kilichopo Mkuza, Kibaha mkoani Pwani juzi. Fatuma amebaki na watoto watatu baada ya mmoja kufariki dunia. Picha na Cosmas Mlekani
Hatari ya ujauzito huo ni ongezeko la siku na kitaalamu mama huyo alipaswa abebe ujauzito kwa wiki 36 na siku mbili au tatu na si siku tano.
Akizungumza katika Kituo cha Afya cha Filbert Bayi Mkuza, Kibaha mkoani Pwani, Dk Amos Katisho alisema mama huyo alijifungua watoto wawili wa kiume na wengine wa kike.
Alisema watoto hao wamezaliwa Oktoba 23, 2023 saa 8:15 usiku katika kituo hicho cha afya kwa njia ya upasuaji uliodumu kwa dakika 45.
“Fatuma alijifungua kwa upasuaji watoto hao, mtoto wa kwanza alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 2.5, wa pili kilo 2.4, wa tatu kilo 2.5 na wa nne kilo 2.2, kitu ambacho sio cha kawaida kwa sababu watoto pacha, hasa wanne wamekuwa wakizaliwa na uzito mdogo,” alisema.
Alisema ongezeko la siku hizo lingesababisha mama na watoto wote kupoteza maisha, lakini ni mtoto mmoja pekee ndiye aliyepoteza maisha.
Alieleza kitaalamu watoto hao huitwa ‘quadruplets’, huku akifafanua maisha ya watoto hao kwamba kila mmoja alikuwa katika mfuko wake na alitumia kondo lake kupata mahitaji kutoka kwa mama, na ndiyo sababu ya kuishi vizuri.
Dk Kitisho alifafanua kuwa, watoto hao walisimama wima walipokuwa tumboni kwa mama yao na ndio kuliwawezesha kukaa kwa nafasi.
“Nilishangaa kuwatoa tumboni watoto wanne, kwani awali kipimo cha ‘ultrasound’ kilionesha ni watoto wawili tu ndio waliokuwepo tumboni, lakini wakati wa upasuaji niliwakuta zaidi,” alisema.
Ni pacha wa mara ya pili
Mama wa watoto hao, Fatuma alimshukuru Mungu, kwani hakutarajia kabisa kubeba ujauzito wa watoto wanne. Alisema hao ni pacha wake wa pili, kwani mara ya kwanza alijifungua watoto wawili.
Baba wa watoto hao, Hussein Mvungi alisema kuwa anamshukuru Mungu na amefurahi kupata watoto hao.
Tukio la kujifungua watoto zaidi ya wawili si la mara ya kwanza, kwani itakumbukwa Machi 2018, Beatrice Mbawala, mkazi wa Dar es Salaam alijifunga watoto wanne katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Pia Machi 2019, Theodora Dickson, mkazi wa Geita alijifungua watoto watatu, huku wawili wakiwa wameungana kuanzia kwenye kitovu hadi kifuani.
Mwaka huo huo, Radhia Solomon (24), mkazi wa Magomeni Chemchem jijini Dar es Salaam, alijifungua watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike.