Furaha, hofu kwa mama wa watoto pacha waliotenganishwa viungo

Hadija Shaban akishukuru Mungu baada ya upasuaji wa kuwatenganisha watoto wake Hussein na Hassan kukamilika salama katika hospitali iliyopo nchini Saudi Arabia. Picha Na Mpigapicha Maalumu

Saudi Arabia/Dar. Mama wa watoto pacha, Hassan na Hussein wa miaka miwili, Hadija Shaban, amesimulia namna alivyoishi na furaha iliyochanganyika na woga kwa zaidi ya saa 16 wakati watoto wake wakitenganishwa katika chumba cha upasuaji.

Watoto hao waliozaliwa mwaka 2021 katika kijiji cha Kifurumo kilichopo Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, walitenganishwa katika upasuaji uliofanyika kwa mafanikio jijini Riyadh, Saudi Arabia, Oktoba 5, mwaka huu.

 Akizungumza na Mwananchi kwa simu kutokea India, Hadija anasema huo ni uzao wake wa pili na kwamba, mtoto wa kwanza ana miaka sita kwa sasa.

"Siku wanatenganishwa nilikuwa na furaha sana, kwa kuwa nilikuwa natamani wanangu waweze kuwa tofauti ili wajitegemee, lakini nilikuwa naogopa mno.

"Namshukuru sana Mungu, watoto wangu wametenganishwa na kwa sasa wanaendelea vizuri, haikuwa rahisi nilikuwa na wakati mgumu sana. Naomba Watanzania wazidi kutuombea," anasema.

 Daktari bobezi wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Zaitun Bokhari alisema watoto hao kwa sasa wanaendelea vizuri.

"Wanaendelea vizuri namshukuru Mungu, leo ni siku ya nne baada ya upasuaji na mpaka sasa bado wako ICU," anasema na kuongeza:

"Wiki moja baada ya kuzaliwa walisogea katika Hospitali ya mkoa wa Tabora wakitokea hospitali ambayo walizaliwa ya misheni ya Nkinga.

"Hospitali ya Nkinga hawakujua kama mama atajifungua watoto walioungana na baada ya kuona hivyo walishtuka na kumpa rufaa kuja Muhimbili akitokea Tabora.

“Kwa kuwa tunafahamiana na hospitali hii ambayo pacha wengine walioungana walifanyiwa upasuaji hapa, tuliwaandikia email (barua pepe) na wakakubali ombi letu na mfalme akaridhia tuwalete watoto huku kwa ajili ya upasuaji tunamshkuru Mungu hili limefanikiwa," alisema Dk Zaitun.

Mpaka wanafanyiwa upasuaji wa kutenganishwa, pacha hao walikuwa na uzito wa kilo 13.5 kwa pamoja na walikuwa wameungana kwenye kifua cha chini, tumbo, nyonga, ini, utumbo, njia ya mkojo na walikuwa kiungo kimoja cha uzazi wa kiume.

Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari nchini Saudia jana, zimeeleza kuwa upasuaji huo ulifanyika Oktoba 5 kwa hatua tisa na timu ya madaktari wabobezi, wataalamu na wauguzi 35 katika hospitali ya watoto ya King Abdullah iliyopo mji wa King Abdulasis chini ya Wizara ya Ulinzi wa Taifa hilo wakiongozwa na Dk Abdullah Rabeen.

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Okiesh akitoa taarifa hiyo, alisema timu ya madaktari wa upasuaji nchini Saudi Arabia, ilitangaza mafanikio ya upasuaji wa pili wa pacha wa Tanzania walioungana.

Operesheni hiyo iliyofanikiwa inafuatia ile ya pacha wengine walioungana kutoka Misenyi, Kagera waliotambulika kwa majina ya Anishia na Melanese, ambao walisafirishwa hadi Ufalme wa Saudi Arabia na kurejea Tanzania baada ya upasuaji uliofanikiwa Agosti 2019.

Kwa mujibu wa Balozi Okiesh, Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Msaada wa Kibinadamu cha Mfalme Salman (KSrelief) na mkuu wa timu hiyo, Dk Abdullah bin Abdulaziz Al-Rabeeah, ameufahamisha ubalozi kuhusu mafanikio hayo.

"Pamoja na ukweli kwamba operesheni ilikuwa ngumu, tumefarijika sana kusikia kuwa upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio," alisema Balozi Okeish.

Alisema kabla ya upasuaji huo, Hassan na Hussein walikuwa wakishiriki sehemu ya chini ya kifua, tumbo na nyonga, kila mmoja akiwa na kiungo kimoja cha chini kwa maana ya njia zote za kujisaidia.

Mapacha hao waliokuwa wameungana pia walikuwa wakigawana kiungo cha tatu cha chini ambacho kilikuwa na ulemavu.


Mafanikio ya Saudi Arabia

Balozi Okeish alisema kabla ya upasuaji wa kuwatenganisha pacha hao, Saudi wa ilishafanikiwa kutenganisha watoto walioungana mara 133 kutoka nchi 24 kwa kipindi cha miaka 33 tangu mwaka 1990 na upasuaji wa watoto hao kutoka Tanzania unakuwa wa 59 hadi sasa.

Mwanadiplomasia huyo alitoa shukrani kwa mlezi wa Misikiti Miwili Takatifu na Mwana Mfalme kwa msaada wao usio na kikomo kwa mpango wa wa kutenganisha pacha walioungana, ambao umeokoa maisha ya watu wengi kote ulimwenguni.

"Msaada wa matibabu ni matokeo ya ushirikiano kati ya uongozi na watu wa nchi hizi mbili,’’ alisema.

Hassan na Hussein waliondoka Tanzania kwenda Riyadh Agosti 23, mwaka huu kwa ndege binafsi baada ya kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa takribani miaka miwili.

Nyongeza kwa msaada wa Mashirika