Ajira migodi mikubwa zafika 15,341
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema katika kipindi cha mwaka 2022, Watanzania 25,341 wamepata ajia kwenye migodi mikubwa ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo 6,668 ndiyo walikuwa wameajiriwa kwenye migodi hiyo huku zaidi ya 8,066 wakipatiwa mafunzo mbalimbali kwenye sekta hiyo.
Arusha. Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema ajira kwa Watanzania katika migodi mikubwa zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia 15,341 mwaka 2022.
Dk Kiruswa ametoa kauli hiyo jana Machi 16, 2023 wakati akizindua rasmi mfumo wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, uzinduzi uliofanyika katika jukwaa la pili la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini linaloendelea jijini Arusha.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2022, Watanzania 8,066 walipatiwa mafunzo mbalimbali katika sekta ya madini na kujengewa uwezo katika utendaji kazi ambapo zaidi ya Sh3.4 bilioni zilitumika.
"Katika mwaka 2022 Dola za Kimarekani 2.2bilioni sawa na asilimia 97.4 ya manunuzi yote ya kampuni za madini yalifanyika kwa kutumia Kampuni za Watanzania, ukilinganisha na Dola za Marekani 238.7 milioni sawa na asilimia 46 ya manunuzi yote kwa mwaka 2018," amesema.
Kuhusu mfumo huo utaibua na kuchochea ongezeko la fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo, uhawilishwaji wa teknolojia, utafiti na maendeleo, matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na Watanzania.
"Suala hili limesababisha sekta ya madini kuwa na mchango mkubwa nchini katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwa fursa nyingi zinatolewa kwa watanzania na kuwapa nafasi ya kukuwa kiuchumi na kiteknolojia," amesema.
"Miongoni mwa changamoto ni baadhi ya kampuni za kigeni kutokuwa tayari kufanya ubia na kampuni za Kitanzania na hivyo kutokidhi matakwa ya Sheria ya Madini. Hii imesababisha kukosa sifa na kushindwa kuidhinishiwa mikataba ya kutoa huduma na bidhaa migodini kwa sasa," ameeleza.
Ametaja changamoto nyingine ni upungufu wa viwanda vikubwa nchini kwa ajili ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini hivyo vinapohitajika migodini huagizwa kutoka nchi za nje kutoka kwa wazalishaji halisi wa mitambo na vipuri.
Kwa upande wake Kamishna wa Madini, Dk Abdulrahman Mwanga amesema lengo la jukwaa ni kuhakikisha wananchi wanatumua fursa zilizopo katika sekta hiyo kwa lengo la kukua kiuchumi.
Kuhusu jukwaa hilo amesema limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuonyesha fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini, kuwajengea uwezo wasambazaji na watoa huduma, kusikiliza changamoto zilizopo katika utekelezaji wa dhana ya ushiriki wa Watanzania na kutatua changamoto zilizopo.