Akili unde iwe mshirika wa vijana, si tishio la ajira
Muktasari:
- Vijana waaswa kuikumbatia AI kuongeza ushindani wa Tanzania.
Morogoro. Vijana wa Tanzania wamehimizwa kujifunza na kutumia teknolojia ya akili unde (AI) ili kujenga ubunifu, kuanzisha biashara na kuongeza ushindani wa nchi katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi duniani.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Koncept Group, Dk Krantz Mwantepele, wakati akitoa mhadhara wa umma ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, ukiwaleta pamoja mamia ya wanafunzi, wahadhiri na wadau wa elimu.
Dk Mwantepele amesema dunia inaingia katika hatua mpya ya maendeleo ya kiteknolojia, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kwa mapinduzi ya nne ya viwanda kwa kuifanya AI kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku na shughuli za kiuchumi.
"Leo hatuzungumzii teknolojia pekee, tunazungumzia mustakabali wa Tanzania. AI isiwe chombo tu unachokitumia, bali iwe mshirika wako wa biashara na ubunifu," amesema.
Amesema AI tayari imeanza kubadili sekta mbalimbali duniani zikiwemo biashara, afya, elimu, fedha, mawasiliano na utawala, hali inayohitaji vijana kuongeza ujuzi wa teknolojia ili wasibaki nyuma katika ushindani wa kimataifa.
Kwa mujibu wa Dk Mwantepele, matumizi sahihi ya AI yanaweza kusaidia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, kuongeza tija katika biashara na kufungua fursa mpya za ajira na ujasiriamali.
Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Koncept Group akitoa Mhadhara wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro kuhusu mapinduzi ya nne ya viwanda kwa kutumia Akili Unde (AI).
Akitoa mfano wa uzoefu wa Koncept Group, amesema taasisi na kampuni zinapaswa kuwekeza katika ubunifu na teknolojia huku vijana wakijifunza kila wakati ili kuendana na mabadiliko yanayotokea duniani.
Mhadhara huo uliambatana na mjadala uliowapa wanafunzi nafasi ya kuuliza maswali kuhusu matumizi ya AI katika biashara, ajira, uongozi na maendeleo ya taifa.
Mhadhara huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi kwa kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kutoka kwa viongozi wa biashara na wataalamu wanaoongoza mageuzi ya kidijitali nchini.
Dk Mwantepele ameendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia na AI nchini na barani Afrika kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga kukuza ubunifu na ushindani wa vijana katika uchumi wa kidijitali.