Akutwa na mihuri ya Serikali akiitumia kuvusha magari mpakani

Muktasari:
- Raia wa Uganda anashikiliwa na Polisi mkoani Kagera kwa tuhuma ya kukutwa na mihuri ya ofisi za serikali aliyokuwa akiitumia kugonga kwenye nyaraka za magari ya mizigo yanayokwenda nchini Uganda kinyume cha sheria.
Bukoba. Jeshi la Polisi mkoani Kagera linamshikilia raia wa Uganda (jina limehifadhiwa), kwa kukutwa na mihuri mitatu ya serikali anayodaiwa kugonga nyaraka za magari ya mizigo yaendayo nchini Uganda kupitia mpaka wa Mutukula wilayani Misenyi.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Septemba 06, 2022 Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, William Mwampaghale amesema, jeshi hilo lilipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo anamiliki mihuri ya mamlaka ya mapato (TRA), ofisi ya kilimo na ofisi ya Tume ya Mionzi (TAEC).
"Tulipata taarifa fiche kuwa mtuhumiwa huyo anamiliki mihuri ya ofisi za serikali na amekuwa akiitumia mihuri hiyo katika shughuli zake kwa kugonga kwenye nyaraka mbalimbali kuonyesha kuwa nyaraka hizo zimeidhinishwa na idara husika ya serikali," amesema Mwampaghale.
Ameongeza kuwa, kutokana na taarifa hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na idara za serikali, waliandaa mtego na Septemba Mosi, 2022 majina ya saa 17:30 katika kitongoji cha Katebe, kijiji cha Mtukula walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na mihuri hiyo.
Amesema, mtuhumiwa huyo alipohojiwa amekiri kumiliki mihuri hiyo na kwamba hadi anakamatwa alishafanikiwa kuvusha magari aina ya Fuso tisa na malori mawili.
Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani taratibu zote za kisheria zitakapokamilika.