Alama ya kumbukumbu ya Kapembe kuwekwa Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasilino na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesimulia namna mwanahabari aliyefariki dunia baada ya kupanda mlima Kilimanjaro alivyotekeleza majukumu yake na kumtengeneza picha zinazoonyesha ana furaha akiwa kileleni.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasilino na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameagiza kuwekwa alama itakayoonyesha mchango wa mwanahabari Joachim Kapembe aliyefariki dunia dunia Desemba 13 maka huu baada ya kushuka Mlima Kilimanjaro.

Akizungumza leo Desemba 17, 2022 wakati wa kongamano la kwanza la maendeleo ya sekta ya habari linalofanyika jijini Dar es Salaam, Nape amesema mwanahabari huyo alifanya kazi kubwa wakati historia ilipoandikwa ya kupandisha mawasiliano kwenye Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi barani Afrika, hivyo ameagiza alama iwekwe kwenye mlima huo.


“Tumeweka rekodi kufikisha mawasiliano kwa urefu ule na Joachim amekuwa sehemu ya historia hii ambayo imeandikwa. Nakumbuka alikuwa mchangafu wakati wote na mwenye nguvu.

“Yeye alitangulia kufika Uhuru Peak, mimi nilifika kwa kuchelewa na aliponiona nakaribia akaandaa kamera ili achukue picha, akagundua nimechoka sana, alisogea pembeni ya kamera na kunionyesha ishara nichangamke,” amesema.

Nape anasema kitendo hicho kilimfanya achangamke na kuwezesha kupatikana kwa picha nzuri ambazo zimesambaa na kumuonyesha Waziri akiwa na nguvu wakati uhalisia haikuwa hivyo.

Waziri amesema tayari ameelekeza mamlaka zinazohusika na Mlima Kilimanjaro kuweka alama itakayoonyesha kumbukumbu ya Joachim katika mlima huo.