Alichokisema Mbowe kuhusu kifo cha Magufuli

Alichokisema Mbowe kuhusu kifo cha Magufuli
Alichokisema Mbowe kuhusu kifo cha Magufuli

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kipindi cha maombolezo ya kifo cha Rais John Magufuli kitumike kufungua ukurasa mpya wa kulirejesha Taifa kuwa moja.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kipindi cha maombolezo ya kifo cha Rais John Magufuli kitumike kufungua ukurasa mpya wa kulirejesha Taifa kuwa moja.

Amesema ana imani rais ajaye atafanikisha kupatikana kwa maridhiano ya kitaifa na Katiba Mpya.

Mbowe ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 18, 2021 katika salamu zake za rambirambi kufutia kifo cha Magufuli kilichotokea jana saa 12 jioni katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika taarifa hiyo Mbowe amesema licha ya kuwa ni wakati wa majonzi na maombolezo ya kitaifa, msiba huo unakumbusha na kutoa fundisho juu ya thamani ya maisha na utu, kuwa na upendo katika kutenda yaliyo mema wakati wa uhai.

“Tunapoendelea na maombolezo tukitumie kipindi hiki kama Taifa kufungua ukurasa mpya wa kulirejesha Taifa kuwa moja na lenye kulinda na kuheshimu uhuru, haki, utu, utawala wa sheria, demokrasia na maendeleo ya watu.”

“Ni imani yetu kuwa rais ajaye atalinda misingi hiyo na ataliongoza kufikia maridhiano ya kitaifa. Tunaamini, kwa kuwa Samia alikuwa makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba atalipatia taifa katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi,” amesema Mbowe.

Ametoa wito kwa wote wenye mamlaka kuheshimu na kulinda matakwa ya sheria na katiba wakati Taifa likipita kipindi kigumu cha mpito na kusisitiza kuwa taarifa za kifo ni nzito kwani ni mara ya kwanza kwenye historia rais kufariki akiwa madarakani.

“Ninatoa wito kwa wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema ndani na nje ya nchi kuiombea familia ya Rais Magufuli wakati inapokabiliana na wakati huu mgumu wa kuondokewa na baba.”

“Aidha, tumuombee mama Samia Suluhu Hassan ulinzi wa Mungu na aweze kusimama katika haki na kweli kwenye kuliponya Taifa,” amesema Mbowe