Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Alichosema Dk Nchimbi akimwakilisha Rais Samia Siku ya Mazingira

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi alivyowasili katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, ikiwa pamoja na kukagua mabanda ya maonesho ya masuala ya mazingira, leo Juni 2026.

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Mazingira, akisema hata hotuba yake amejitahidi kuisoma 'kirais-rais.'

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ametaka utoaji wa vibali vya ujenzi nchini uambatane na sharti la upandaji miti mitano ili kutunza na kuhifadhi mazingira.

Katika hotuba yake, aliyosema anaizungumza kwa kuwa anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Dk Nchimbi amesisitiza pia umuhimu wa usimamizi wa mifumo ya taka.

Dk Nchimbi ametoa hotuba hiyo jijini Dodoma leo, Ijumaa, Juni 5, 2026, wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Mazingira, alikokuwa mgeni rasmi badala ya Rais Samia.

Aliianza hotuba hiyo kwa kueleza kuwa Rais Samia ndiye alipangwa kuwa mgeni rasmi, lakini ugumu wa ratiba ya mkuu huyo wa nchi umelazimu awakilishwe naye.

Amesema Rais Samia amesafiri kwenda Russia kwa shughuli za kikazi na zenye umuhimu kwa Taifa na hivyo, hata mamlaka ya urais amemwachia yeye.

“Mheshimiwa Rais ameenda safari kuwakilisha Taifa letu kwenye safari muhimu sana ya kikazi nchini Russia na mamlaka ya urais nayo akanikabidhi,” amesema.

Rais Samia yuko nchini Russia kwa ziara ya siku tatu. Katika ziara hiyo amefanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Amesema kitendo cha Rais Samia kumtuma yeye (Nchimbi) kumwakilisha kwenye tukio hilo na kumkabidhi mamlaka kwa siku ambazo mkuu wa nchi hayuko nchini, kumeipa heshima ofisi yake.

“Bado ameipa heshima kubwa ofisi yangu, lakini ameipa heshima kubwa Siku ya Mazingira,” amesema.

Akianza kusoma hotuba hiyo, Dk Nchimbi amesema kwa kuwa anazungumza kumwakilisha mkuu wa nchi, atajitahidi kuongea kirais-rais.

“Kwa kuwa namwakilisha Mheshimiwa Rais, nitajitahidi kuongea kirais-rais, nitaisoma hotuba yake kama ilivyo,” amesema.

Akisoma hotuba ya Rais Samia, amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 67 na ifikapo mwaka 2050, idadi inakadiriwa kufikia watu milioni 118.

Ongezeko hilo, amesema, litasababisha mahitaji ya kuwepo kwa rasilimali nyingi muhimu zinazohitaji mazingira bora, ikiwemo ardhi, maji, nishati, mifumo ya elimu na usafirishaji, ndiyo maana Dira ya 2050 imejumuisha masuala ya mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Amewataka wadau wa mazingira kuunga mkono jitihada za Serikali kutekeleza afua zote za mazingira zilizoelezwa katika programu hiyo.

Ametaka mamlaka za serikali za mitaa kuanzisha bustani za kijani na kuhakikisha zinatunzwa, mamlaka zinazotoa vibali vya ujenzi kuweka sharti na kusimamia ili kila kibali kinachotolewa kiambatane na agizo la kupanda miti isiyopungua mitano.

Ametaka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha uwepo wa miche ya kutosha ili kurahisisha upandaji miti nchini.

Dk Nchimbi ameielekeza Ofisi ya Makamu wa Rais kubainisha misitu inayofaa na kuisajili katika biashara ya kaboni.

Ameitaka Wizara ya Ardhi kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ili kupunguza changamoto ya uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya ardhi yasiyo endelevu.

Pia, ametaka mamlaka za serikali za mitaa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa taka, hasa kuanzisha vituo vya kuchakata taka ili kupunguza kiasi cha taka kwenye madampo na kuchangia urejelezaji.

Agizo lingine alilitoa kwa taasisi za utafiti kufanya utafiti kuhusu mimea na viumbe vamizi vinavyozidi kuongezeka na kuathiri mifugo na mimea mingine katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk Nchimbi, wakati anahitimisha hotuba yake, alimwita mtoto Jackline Elihabi, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Maninga, aliyetoa wasilisho kuhusu utunzaji wa mazingira.

Katika wasilisho hilo, Jackline alieleza namna ya kutunza mazingira kupitia njia tatu za uchumi ambazo ni uchumi wa moja kwa moja, uchumi wa kuchakata na uchumi mzunguko.

Amesema uchumi wa moja kwa moja na wa kuchakata ni hatari kwa mazingira, akisisitiza utumiwe uchumi mzunguko ambao hauzalishi kabisa taka. Hatua hiyo iliibua shangwe ukumbini, ishara ya kumsifu mtoto huyo.

Baada ya wasilisho hilo, Dk Nchimbi alisema, “Niliona kwa kuwa mwakilishi wa Mheshimiwa Spika (Spika wa Bunge, Mussa Zungu) yupo, ikitokea huko kuna mbunge hatoshitoshi, anaweza akaziba pengo huyu (Jackline),” amesema.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni, amesema mipango ya Serikali ni kuhakikisha miaka 25 ijayo Tanzania inakuwa na miti ya kutosha.

Pia, amesema katika kipindi hicho matarajio ni kuwa na Tanzania yenye ongezeko la matumizi ya nishati safi na itakuwa na udhibiti wa ukiukwaji wa mazingira, ikiwemo kudhibiti kelele kwenye makazi ya watu.

Matarajio mengine, amesema, ni kupatikana kwa fursa katika sekta ya mazingira ili kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa chanzo cha tatu kikubwa cha mapato nchini.

Amesema programu hiyo inatarajiwa kutumia Sh7 trilioni zitakazotoka Serikalini, sekta binafsi, washirika wengine wa maendeleo na asasi za kiraia.