Alivyomwagiwa chai ya moto kwa kudai talaka

Alivyomwagiwa chai ya moto kwa kudai talaka

Muktasari:

Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu dunia ihitimishe siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Mariam Msafiri amemaliza mwaka vibaya kufuatia majeraha makubwa yaliyotokana na kumwagiwa chai ya moto na mumewe.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu dunia ihitimishe siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Mariam Msafiri amemaliza mwaka vibaya kufuatia majeraha makubwa yaliyotokana na kumwagiwa chai ya moto na mumewe.

Mariam (25) mkazi wa Mbande Kisewe na mama wa watoto watatu, alikumbwa na kadhia hiyo asubuhi ya Desemba 17 mwaka huu wakati akiandaa chai kwa ajili ya kifungua kinywa cha familia yake.

Akizungumza na Mwananchi Mariam alieleza kuwa kabla ya tukio hilo mara kadhaa amekuwa na migogoro na mume wake aliyemtaja kwa jina la Seif Abdul lakini siku hiyo alifikia hatua ya kumwagia chai iliyokuwa inachemka jikoni.

Anasema, “Kabla ya siku hiyo tulikuwa na ugomvi chanzo ni kwamba ana mwanamke mwingine na nikamwambia kama vipi anipatie talaka ili tuachane kwa usalama, akanipeleka hadi kwao kwa madai anakwenda kunikabidhi talaka yangu lakini hakufanya hivyo akaniacha huko, akatokomea.’’

Aliongeza: ‘‘Kwa kuwa nyumbani kwao na tunapoishi sio mbali ,nilirudi nyumbani kwangu nikalala na watoto wangu, yeye hakurudi siku hiyo. Asubuhi nikaamka kuendelea na shughuli zangu kama kawaida ikiwamo kuandaa kifungua kinywa. Nilibandika chai kwenye jiko la gesi.’’

Mariam alisema kuwa mumewe alirejea asubuhi hiyo wakaanza mizozo tena, ndipo alipomtamkia wazi kwamba yuko tayari kumuacha ila lazima amuachie kilema.

“Aliponiambia hivyo ndipo akachukua ile chai iliyokuwa jikoni lengo lake animwagie usoni, niliwahi kukinga mkono ikasaidia kuzuia isiende usoni; matokeo yake nikaungua kwenye mkono wa kushoto kama hivi unavyouona.’’

Mariam anasema hii si mara ya kwanza kufanyiwa ukatili kwani mara kadhaa amekuwa akipigwa kwa mikanda, nondo wakati mwingine kuchomwa kwa bisibisi, lakini alikuwa akivumilia kwa sababu hakutaka kuwaacha watoto wake wateseke.

Pamoja na vipigo alidai kuwa wakati mwingine mumewe alikuwa hamwachii fedha ya chakula, licha ya kufahamu kuwa ananyonyesha mtoto mdogo wa miezi saba jambo lililochangia afya yake kudhoofika.

Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia mwili wa Mariam ukiwa na makovu kadhaa hasa kwenye miguu na mgongoni ambako anadai amekuwa akipigwa kwa kutumia mikanda.

Mariam alieleza hayo ikiwa ni muda mfupi tangu alipotoka kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Pugu alipopewa dawa kadhaa za maumivu na kutibu majeraha.

Baba mzazi wa Mariam, Paulo Msafiri alikiri kupata malalamiko kutoka kwa mtoto wake dhidi ya manyanyaso aliyokuwa anapata kwa mumewe lakini alikuwa akimwambia avumilie kwa sababu hakufahamu undani wa hayo.

“Mwanangu alikuwa anapiga simu kuelezea migogoro yao na mimi kama mzazi nilikuwa namsihi awe mvumilivu, kumbe haniambii ukweli kwamba anakutana na unyama wa aina hii.

‘‘Kwa kiasi fulani najilaumu kwamba nimechangia kufikia hatua hii, kwani ule uvumilivu niliokuwa namsisitiza mwanangu matokeo yake ni haya, anapata ulemavu na hata afya yake imedhoofika sana,”alisema.

Kwa mujibu wa baba huyo amejaribu kumtafuta mkwe wake bila mafanikio na tayari wamesharipoti kituo cha polisi Gongo la Mboto kuhusu tukio hilo akisisitiza kuwa lazima sheria ifuate mkondo wake.

‘‘Ombi langu kwa hizi taasisi zinazohusika na haki za binadamu zimsaidie huyu binti yangu, sheria ifuate mkondo wake. Yule kijana inaonekana ana matatizo kwa sababu awali walikuwa wakikorofishana kidogo anamuandikia talaka hadi zikafika tatu, ndoa ikawa imefikia ukomo akaja kuomba kwa barua kabisa kwamba hawezi kurudia tena anamtaka mkewe, zile talaka zikachomwa halafu leo anamfanyia unyama wa aina hii,” alisema baba huyo huku uso wake ukiwa umetanda huzuni.

Juhudi za kumpata mumewe hazikufanikiwa baada ya kutafutwa kwa simu pasipo mafanikio huku akiwa hapatikani nyumbani.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga alisema wanawake wanapaswa kukataa ukatili bila kuangalia mambo yanayowazunguka yakiwamo ya familia.