Aliyeahidiwa cherehani na Rais Samia, afunguka

Muktasari:
- Bahati ya mwezio usilalie mlango wazi, ndivyo unavyoweza kusema juu ya mshonaji wa nguo mbalimbali Beatrice Mwalingo (28) ambaye ameahidiwa kununuliwa cherehani na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Beatrice Mwalingo (28) anayejishulisha na ushonaji nguo amesema hakuamini kama Rais Samia Suluhu Hassan atajibu ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa Instagram na akaahidiwa kumnunuliwa cherehani na kiongozi huyo.
Beatrice anayefanya kazi ya ushonaji kwa miaka mitano sasa Kivule Dar es Salaam, aliomba zawadi ya cherehani kwa Rais Samia kupitia ukurasa wa kiongozi huyo wa Instagram.
Awali Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika juu ya kuwasili kwake nchini Indonesia kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu, kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo.
“Uhusiano wa Tanzania na Indonesia ambao mapema mwezi huu (Januari 13, 2024) ulitimiza miaka 59, umekuwa wenye tija kwa nchi yetu na mamilioni ya Watanzania hasa kwenye kilimo na biashara. Tunaendelea kuifanya kazi ya kukuza uhusiano huu ili kuleta tija zaidi kiuchumi kwa nchi yetu,” aliandika Rais Samia.
Hata hivyo, Beatrice yeye pasipo kujua itakuwa siku yake ya bahati aliacha ujumbe chini ya chapisho hilo uliosomeka. “Sawa mama. Ukiwa unarudi nyumbani naomba uniletee zawadi ya cherehani,” aliandika.
Muda mchache baadaye Rais Samia alijibu ujumbe wake na kumuambia. “Hujambo, Beatrice? Nimepata wasaa wa kuusoma ujumbe wako. Hongera kwa kazi na kujituma. Wasaidizi wangu watawasiliana na wewe kukusaidia upate mashine uliyoomba kwa shughuli zako. Nakutakia kila la kheri.”
Akizungumzia na Mwananchi leo, Alhamisi Januari 25, Beatrice amesema cherehani hiyo itakuwa ni mwanzo wa kuwezesha vijana wengine ili wajikwamue kimaisha.
"Ukweli siku ya jana wakati nimekaa nilisema ngoja niombe cherehani kwa mama na kweli sikutegemea kama nitajibiwa, ukweli nimefurahi sana ni kitu ambacho kimenipa furaha na motisha kwenye kazi zangu zaidi,” amesema.
Beatrice anasema taarifa za kujibiwa na Rais Samia alizipata kutoka kwa rafiki yake, lakini hakutaka kumuamini hadi alipoona mwenyewe.
Licha ya kujibiwa anasema kuwa bado hajatafutwa, lakini anaamini watafanya hivyo kwani muda bado.
Amewashauri watu kujaribu kueleza changamoto zao kwenye post za viongozi kwani hawawezi kujua bahati zao.
Katika uzoefu wake, Beatrice amesema awali alikuwa akifanya kazi nchini Japan, lakini tangu Novemba mwaka jana alirudi Tanzania kuendelea na kazi hiyo.