Haya hapa mambo muhimu mazungumzo ya Rais Samia na Widodo wa Indonesia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Mhe. Joko Widodo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 22 Agosti, 2023.
Muktasari:
- Viongozi wakuu wa nchi za Tanzania na Indonesia wamekubaliana kuboresha maeneo mbalimbali ikiwemo ya afya, umeme na madini, sambamba na kuimarisha sekta za viwanda na biashara.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema wamekubaliana na Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Joko Widodo kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi.
Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania na Indonesia zimedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano katika viwanda, kilimo, nishati, mafuta na gesi, uvuvi, utalii sambamba na kubadilisha maarifa na teknolojia.
Ameeleza hayo leo Jumanne Agosti 22, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari akiwa na mgeni wake, Rais Widodo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Rais Samia amesema katika mazungumzo yao ya faragha na mgeni wake huyo, alimueleza nia ya Tanzania kupata uzoefu kuhusu uzalishaji wa mafuta ya mawese, akisema Indonesia ni mzalishaji mkubwa wa mafuta hayo duniani.
“Kama mnavyofahamu Serikali imejidhatiti kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia ili kuacha kutumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa hiyo toka nchi za nje.
“Pia nimemuomba Rais Widodo ushirikiano katika kujenga uwezo wa kiufundi kwenye maeneo ya sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa,” amesema Rais Samia.
Mbali na hilo, Rais Samia amesema “Katika mazungumzo yetu na Rais Widodo amependekeza ndani ya siku 90 tuzungumze na kukubaliana kuhusu makubaliano na ushirikiano mkubwa kati ya mataifa haya mawili, nimekubali hilo. Matumaini yangu katika makubalianao haya nchi zetu zitakuwa na sura mpya wa kina na mpana zaidi kwa manufaa pande zote mbili,"amesema.
Naye, Rais Widodo amesema anajisikia faraja kutembela Tanzania kwa mara kwanza, akisema nchi yake imekuwa na historia ndefu na imara na Mataifa ya Afrika tangu mwaka 1955.
Rais Widodo amesema Indonesia itashinikiza uwepo wa mkataba wa kipambele wa ushirikiano na Tanzania ili kuhakikisha utekelezaji wa mkataba wa makubaliano baina ya mataifa hayo mawili.
“Pia Indonesia inakusudia kuongeza uwekezaji ikiwemo katika sekta ya gesi asilia. Indonesia itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika na sasa ipo kwenye hatua za mwisho za uandaaji wa mpango wa maendeeo wa ushirikiano na nchi za Afrika,” amesema.
Awali kabla ya Rais Samia na Widodo kuzungumza, mawaziri na watendaji wakuu taasisi za sekta za umeme na gesi wa Tanzania na Indonesia walisaini mikataba saba ya makubalianao na ushirikiano baina ya mataifa hayo.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja kuboresha sekta za nishati, umeme, madini sambamba na kuanzisha Tume ya pamoja ya ushirikiano baina ya nchi mbili.
Pia, mkataba wa makubaliano kuhusu kuondoa visa kwa wamiliki wa pasipoti za kidiplomasia na nyingine, na kuanzisha ushirikiano katika uboreshaji wa sekta afya.