Mikakati ya Bodi ya Korosho 2025/2026

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred akizungumza na viongozi pamoja na wadau wa korosho, jinsi walivyojipanga kufikia malengo ya kuzalisha korosho kufikia Tani laki saba kwa msimu wa mwaka 2025/2026 kuzalisha .Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Kwa mwaka 2024/2025, uzalishaji wa korosho mkoani Lindi umeongezeka na kufikia tani 528,000.
Lindi. Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), imejipanga kuhakikisha inafikia lengo lililowekwa na Serikali la kuzalisha tani 700,000 za korosho kwa mwaka 2025/2026.
Akizungumza leo Ijumaa Julai 4, 2025, kwenye kikao cha maendeleo ya tasnia ya korosho kwa Mkoa wa Lindi kuelekea msimu wa mauzo wa 2025/2026, Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred, amesema bodi hiyo imejipanga kusambaza viuatilifu mapema ili kuwasaidia wakulima kuanza kupulizia mikorosho kwa wakati na hivyo kufikia malengo ya uzalishaji.
“Hadi sasa tumeshaanza kusambaza viuatilifu kwa Mkoa wa Lindi na tunaendelea kugawa. Naomba wakulima ambao hawajajisajili wafanye hivyo ili wapate viuatilifu na dawa za maji. Hadi sasa zaidi ya viuatilifu 7,000 na dawa za maji zaidi ya 300,000 tumeshaanza kugawa kwa wakulima. Hii itasaidia mikorosho kutopata magonjwa,” amesema Alfred.
Ameongeza kuwa usambazaji wa viuatilifu mapema pamoja na utoaji wa elimu kwa wakulima kutasaidia kuongeza uzalishaji na kufikia malengo.
“Tumefanya jitihada kubwa kwa vijana wa Jenga Kesho Bora (BBT). Tumewapa mafunzo na watatusaidia kusimamia wakulima na kutoa elimu ya kutosha. Pia nawaomba wanunuzi, mwaka huu hakuna atakayekosa mzigo kwani kutakuwa na utaratibu wa kukagua mizigo kwenye maghala kabla ya kuingia sokoni,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack amewataka wakuu wa wilaya kushirikiana na maofisa kilimo kuanzisha mashamba mapya ya mikorosho ili kuongeza uzalishaji kwa tija.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa korosho kuelekea kwenye msimu wa mauzo ya korosho 2025/2026. Picha na Bahati Mwatesa
Naye mkulima kutoka Liwale, Abraham Jumbe ameipongeza Bodi ya Korosho kwa kuanza kusambaza viuatilifu mapema, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji.
Kwa mwaka 2024/2025, uzalishaji wa korosho katika Mkoa wa Lindi umeongezeka na kufikia tani 528,000.