Aliyedaiwa kumuua trafiki aachiliwa huru
Mshtakiwa Aman Elikana, aliyekuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya askari Polis kikosi Cha Usalama Barabara akilia baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Uamuzi wa kumwachia huru umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Romuli Mbuya, akisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Aman Elikana (38) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Elikana alikuwa akituhumiwa kumuua askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, mwenye namba D8254 Sajenti Mensah kwa kumpiga risasi kifuani iliyomvunja mbavu upande wa kulia na kutoboa mapafu.
Ilidaiwa kuwa mauaji hayo yalifanyika katika mataa ya kuongozea magari eneo la Sayansi, Kijitonyama.
Uamuzi wa kumwachia huru umetolewa leo Jumatatu Machi 20, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Romuli Mbuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.
"Upande wa mashtaka imeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo, hivyo mahakama ina muachia huru Aman," amesema Hakimu Mbuya.