Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyegomea uteuzi asimamishwa kazi CWT

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT), Japhet Maganga.

Muktasari:

  • Mbali ya hilo, viongozi 10 Maganga akiwamo walikamatwa na Polisi juzi wakidaiwa kufanya vurugu kwenye mkutano wa CWT uliofanyika katika ukumbi wa St Gasper jijini Dodoma.

Dodoma. Baraza la Kuu la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) limemsimamisha ukatibu mkuu Japhet Maganga.

Hatua hiyo inatokana na mwajiri wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kumfukuza kazi.

Mbali ya hilo, viongozi 10 Maganga akiwamo walikamatwa na Polisi jana wakidaiwa kufanya vurugu kwenye mkutano wa CWT uliofanyika katika ukumbi wa St Gasper jijini Dodoma.

Rais wa CWT, Leah Ulaya amesema hayo leo Februari 17, 2024  baada ya baraza hilo kufikia maamuzi hayo.

Amesema baraza kuu lilitaka kufahamu namna ambavyo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilivyokuwa vikiripoti kuhusu Maganga kushindwa kupata kibali kutoka kwa mwajiri wake cha kufanya kazi CWT.

Amesema baraza hilo lilijadili hoja hiyo kwa lengo la kuondoa sintofahamu iliyokuwapo.

 Leah amesema baraza hilo limeona kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Maganga hawezi kuendelea kutumikia nafasi ya ukatibu mkuu wa CWT.

“Baraza limeona mamlaka yake ya ajira ilishamtoa kwenye ajira, yaani amefukuzwa kazi kwa mujibu wa barua ambayo tumeisoma (katika kikao), iliyotoka katika mamlaka yake ya ajira Temeke (Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam).”

“Kwa muktadha huo baraza limeona halikuwa na haja ya kuendelea kunyamaza na limefikia maamuzi kuwa hawezi kuwa tena Katibu Mkuu wa CWT labda kutokee mambo mengine kadri itakavyokuwa mbele,” amesema.


Ilivyokuwa

Amesema walipokuwa wakiahirisha kikao Alhamisi walipanga kujadili hoja ya kibali cha Maganga na walipofika Ijumaa walianza na hoja hiyo, kama walivyokuwa wamepanga.

“Aliyekuwa Katibu Mkuu wa kikao hicho akaibua hoja kuwa hana imani na mimi (Leah) kuongoza kikao hiki, ndipo wajumbe wakaibua molari ya kusema kwa nini Rais na mwenyekiti wetu akataliwe kuongoza kikao,” amesema.

Amesema hilo lilizua tafrani, hivyo ilikuwa ngumu kupima kila mtu alikuwa na hisia gani na kwamba vyombo vya usalama viliingilia kati ili kutuliza fujo hiyo.

Leah amesema walichokifanya baadhi ya wajumbe ni kumtoa Maganga ambaye anafikiri alikuwa katika tafrani ndani ya ukumbi huo.

“Ilipotokea vurugu wajumbe walianza kuvutana huku na kule, hakuna mtu ambaye alikuwa anahisi ni nini kilikuwa kinatokea. Lakini tulifuatilia kwa nini waliendelea kuwa kule (Polisi),” amesema.

Amesema vyombo vya usalama vilisema hawawaweki huko kwa sababu ya adhabu bali kwa kuwa kikao kinaendelea itakuwa si vyema kuwaachia.

Leah amesema baada ya kutoa taarifa kuwa kikao kimemalizika jana, anadhani kuwa wataachiwa huru.

Amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni Kizito Shuli, Alistida Ishengoma, Leonce Mwalatishi, Alphonce Mbasa, Costa Paulo, Hamis Mtundua, Hamisi Chinahova, Daud Mafwili na Kiyola Mahanya.

Mbali na hayo, amesema baraza limewarejesha kwenye uanachama na uongozi wanachama 18, waliofutiwa uanachama Juni 18, mwaka jana baada ya kuonekana kuvunja katiba ya chama hicho.


Kauli ya Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema wanachama hao walikamatwa katika mkutano wa chama hicho jana baada ya kupata taarifa kuhusu vurugu.

“Tulipata taarifa kuwa kuna watu wanafanya fujo tukaenda kudhibiti kabla hayajatokea madhara kwenye mkutano huo. Sisi hatujui ilikuwaje zikatokea fujo waulizwe CWT wenyewe,” amesema.

Katika ukumbi huo  kuliwa na Polisi waliokuwa wakirandaranda hadi kikao kilipoisha.

Hata hivyo, alipoulizwa Leah amesema ni kawaida ya mikutano ya chama hicho kuwa na ulinzi.


Wito kurejea kazini

Oktoba mwaka jana uongozi wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ulitoa tangazo katika ukurasa wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kumtaka Maganga arejee katika kituo chake cha kazi.

Katika tangazo hilo, ilionyesha kuwa Maganga aliomba kibali cha kuazimwa na CWT kwa mara ya kwanza Agosti 2017 kilichomalizika Septemba 30, 2020.

Maganga aliomba nyongeza ya kibali cha kuazimwa Juni Mosi mwaka 2020 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi alimpa nyongeza hadi Agosti 10 mwaka 2020 kilichoishia Septemba 30, mwaka jana.

Tangazo hilo lilisema Maganga ambaye cheo chake ni mwalimu mwandamizi, aliomba tena kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu lakini Katibu Mkuu Utumishi hakuridhia maombi hayo.

“Hivyo basi Mwalimu Japhet Maganga anapaswa kurejea kwenye kituo chake cha kazi mara moja Oktoba Mosi, 2023,” lilisema tangazo hilo.

Desemba 5, mwaka jana uongozi wa Manispaa ya Temeke ulitoa barua ukieleza Maganga amesimamishwa kazi kwa tuhuma za utoro kazini, kukaidi na kukataa maelekezo halali ya viongozi wake.

Akijibu hayo, Desemba 7 mwaka jana Maganga alieleza kushangazwa na barua hiyo kwani yeye ni mwajiriwa wa mkataba wa kudumu wa CWT.

Maganga alisema kinachofanyika ni vita ya madaraka na walioondolewa kwenye uongozi.

Alisema yeye alikoma kupokea mshahara na marupurupu yote kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tangu Desemba 2017 baada ya kuajiriwa kwenye nafasi ya uhasibu makao makuu ya CWT.

“Unanisimamishaje kwa kazi ambayo sina haja nayo. Kama ni mtoro kazini, sheria inasema mtumishi akikosekana kazini siku tano, amejifukuzisha kazi. Mimi sijaripoti tangu waliposema Oktoba Mosi, wamalize kazi,” alisema.

Maganga aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukatibu mkuu alichaguliwa mwaka jana kushika nafasi ya ukatibu mkuu baada ya chama hicho kumvua uongozi, Deus Seif.

Januari 25 mwaka jana, Maganga na Makamu wa Rais, Dinna Mathaman na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya, lakini ni Dinna pekee aliyeenda kuapa kushika nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Leah aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakati Maganga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.