Aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kuua wawili aachiwa huru
Muktasari:
- Shabani Juma, alishtakiwa, kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya mauaji ambapo katika uamuzi wa Mahakama ya Rufaa umeeleza kutokana na dosari za kisheria inabatilisha mwenendo, hukumu na kuamuru mrufani aachiwe huru.
Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa Shabani Juma, aliyekutwa na hatia ya mauaji ya watu wawili, kufuatia dosari za kisheria zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Shabani alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya mauaji ya Milembe Zengo na Kwangu Zengo, Mei 11, 2008 katika Kijiji cha Idukilo, Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Dk Ubena Agatho, walioketi Tabora, walitoa hukumu hiyo iliyomuachia huru Shabani Juni 26, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Mkuye amesema baada ya kupitia mwenendo na kupitia hoja za pande zote mbili, wamejiridhisha kuwa wazee wa baraza na Jaji aliyesikiliza kesi ya msingi, waliwauliza maswali mashahidi wa upande wa mashtaka, wakati hawaruhusiwi kuwahoji mashahidi lakini wanaruhusiwa kuuliza maswali kwa ufafanuzi.
Amesema haikuwa sahihi wazee wa baraza na Jaji kuwahoji mashahidi na ulikuwa ukiukwaji wa utaratibu ambao hauwezi kutibika kwani ulifikia ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa kwa mrufani, hivyo kufanya shauri na hukumu kuwa batili.
Shabani alipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka mawili ya mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Mrufani huyo alikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wawili.
Rufaa
Baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, Shabani alikata rufaa Mahakama ya Rufaa akiwa na sababu mbili ambazo ni Mahakama ilikosea kuruhusu wazee wa baraza na yeye mwenyewe kuwahoji mashahidi kwa kukiuka kanuni zilizowekwa za mashauri ya haki.
Nyingine ni maelezo yake ya onyo yaliyopokelewa kimakosa kama kielelezo cha kwanza yalikubaliwa mahakamani katika ushahidi na Jaji alikosea kisheria kutegemea ushahidi wa shahidi wa pili kumtia hatiani.
Katika rufaa hiyo Shabani aliwakilishwa na Wakili mmoja huku Jamhuri ikiwakilishwa na wakili Enosh Gabriel.
Wakili wake aliieleza mahakama kuwa wazee wa baraza na jaji aliyesikiliza kesi hiyo waliwahoji mashahidi kimakosa ambapo aliielekeza mahakama ukurasa wa 58 hadi 63 wakati shahidi wa kwanza akitoa ushahidi, Jaji na wazee wa baraza waliwahoji mashahidi.
Wakili huyo amesema kuwa suala hilo lilimtokea pia wakati shahidi wa pili kama inavyoonyeshwa kwenye ukurasa wa 63 wa rekodi ya rufaa ambayo ilikuwa ni kinyume na kifungu cha 290 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ambayo hairuhusu shahidi kuhojiwa na aidha mshauri au mahakama.
Wakili huyo alisisitiza kuwa, chini ya kifungu hicho cha sheria, mashahidi wa upande wa mashtaka wanahojiwa na mtuhumiwa au wakili wake peke yake na kuwa wazee wa baraza wanaruhusiwa tu kuuliza swali ili kupata ufafanuzi chini ya kifungu cha 177 cha Sheria ya Ushahidi.
Wakili huyo alihitimisha kwa kuiomba Mahakama ione kuwa ukiukwaji huo ni mbaya na kufanya shauri na hukumu yake kuwa batili na kuomba Mahakama hiyo isitumie kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura ya 141 (AJA), kubatilisha mwenendo na hukumu yake na kutoa amri ya kusikilizwa upya kuanzia mashahidi.
Kuhusu maelezo ya onyo ya mrufani alieleza kuwa yalirekodiwa nje ya muda na shahidi wa kwanza ambaye alienda kumchukua mrufani Kahama bila kutaja muda aliokwenda huko na aliporudi naye Kituo cha Polisi Kishapu.
Alidai kuwa taarifa iliyorekodiwa nje ya muda ilikiuka kifungu cha 51 (1) (a) cha CPA na kwa hivyo, haifai kupokelewa kwa ushahidi na dawa ya ukiukwaji huo ni kuufuta kwenye rekodi na kuwa iwapo yatafutwa hakuna ushahidi mwingine wa kuendeleza hukumu hiyo na kuomba mahakama kuruhusu rufaa na kumwachia huru mrufani.
Wakili wa Jamhuri alikubaliana na hoja ya wakili wa mrufani kuwa ni makosa kwa wazee wa baraza kuhusu maelezo ya onyo alipinga na kueleza kuwa maelezo hayo yalirekodiwa ndani ya muda.
Amesema kuwa kuagiza kusikilizwa upya kutaruhusu upande wa mashtaka kujaza mapengo na kuomba mahakama ifute hatia dhidi ya mrufani na kumwachia huru.
Uamuzi wa majaji
Jaji Mkuye amesema kutokana na mawasilisho ya pande zote, kupitia mwenendo, suala la uamuzi wa Mahakama hiyo ni wapo mashahidi walihojiwa na wazee wa baraza na Jaji.
Amesema kama ilivyowasilishwa na mawakili wote wawili, wazee wote wa baraza na jaji waliwauliza maswali mashahidi wa upande wa mashtaka, wakati hawaruhusiwi kuwahoji mashahidi, ila wanaruhusiwa kuuliza maswali kwa ufafanuzi.
Katika kuhitimisha hoja hiyo, majaji hao walieleza kuwa haikuwa sahihi wazee wa baraza na Jaji kuwahoji mashahidi na ulikuwa ukiukwaji wa utaratibu kwani ulifikia ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa kwa haki kwa mrufani.
“Kwa kweli, ukiukwaji huo unafanya shauri na hukumu inayotokana kuwa batili. Kwa hiyo, tunabatilisha, tunafuta hukumu na kuweka kando hukumu iliyotolewa kwa mrufani,” amesema Jaji Mkuye.
Jaji huyo amesema kwa kawaida suluhu ingekuwa ni kubatilisha mwenendo wa kesi na hukumu kisha kutoa amri ya kusikilizwa upya kwa kesi hiyo, ila kutokana na mawasilisho ya mawakili amri hiyo haiwezi kuwa chaguo bora kutokana na upungufu wa ushahidi ambao ulitegemewa na mahakama kumtia mrufani hatiani.
Amesema katika kesi hiyo, ushahidi uliotegemewa kumtia hatiani mrufani ulitoka kwa mashahidi wawili ambao walikuwa mpelelezi wa kesi hiyo na maelezo ya onyo ya mrufani.
Kuhusu maelezo ya onyo, ameema shahidi wa kwanza alieleza Mei 10, 2008 kuwa akiwa na maofisa wengine wa polisi walienda katika eneo la tukio mauaji yalipotokea na kuwa Septemba 6, 2008 alipata taarifa za watu watatu waliokamatwa kwa tuhuma za wizi wa mbuzi ila uchunguzi ulibainisha mmoja wao (mrufani) alihusika na mauaji ya awali.
Jaji amesema shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa alikwenda Kituo cha Polisi Kahama ambako aliwakusanya watuhumiwa watatu akiwamo mrufani, hata hivyo, hakueleza tarehe aliyokwenda huko na kurejea na mrufani Kituo cha Polisi Kishapu.
Kuhusu shahidi wa pili, amesema Septemba 18, 2008 alienda kuandika maelezo ya onyo ya mrufani katika Kituo cha Polisi Kishapu, ambayo mrufani huyo alieleza kukamatwa Agosti 3, 2008 ila haijulikani ni wapi alikuwepo hadi Septemba 18, 2008 alipoandika maelezo hayo ya onyo.
“Inaleta shaka kwa kuzingatia dosari zilizoonyeshwa na wakili wa mrufani katika ushahidi wa upande wa mashtaka ambao tunaona kuwa unaweza kudumu, tunadhani, amri ya kusikilizwa upya haitakuwa chaguo bora kwa kuwa upande wa mashtaka unaweza kutumia fursa hiyo kujaza mapengo.
“Kwa hivyo, tunaruhusu rufaa na kuamuru kwamba mrufani aachiliwe mara moja isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu nyinginezo halali,” amehitimisha.