Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyehukumiwa kwa kuvunja, kuiba mahakamani aachiwa huru

Muktasari:

  • Hukumu hiyo ilitolewa Julai 3, 2026 na Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Moshi, ambaye alibatilisha uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai na kuagiza Judika aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.



Arusha. Ni nadra kusikia Mahakama, chombo kinachosimamia utoaji wa haki ikiwa mwathirika wa wizi.

Hata hivyo, licha ya Judika Nkya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuiba mali za Mahakama ya Mwanzo ya Bomang'ombe zenye thamani ya Sh2.42 milioni, Mahakama Kuu imefuta hukumu hiyo baada ya kubaini upande wa mashtaka haukuthibitisha hatia yake bila kuacha shaka.

Hukumu hiyo ilitolewa Julai 3, 2026 na Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Moshi, ambaye alibatilisha uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai na kuagiza Judika aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.

Awali, Judika alikuwa amepatikana na hatia ya makosa mawili; kuvunja jengo kwa nia ya kutenda kosa kinyume na Kifungu cha 296(a) na (b) cha Kanuni ya Adhabu na wizi kinyume na Vifungu vya 258(1), 258(2)(a) na 265 vya sheria hiyo.

Katika shtaka hilo, ilidaiwa kuwa Septemba 30, 2024 alivunja Mahakama ya Mwanzo ya Bomang'ombe iliyopo Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro na kuiba fedha taslimu Sh700,000, kompyuta ya mezani aina ya Dell yenye thamani ya Sh1.2 milioni, skana yenye thamani ya Sh500,000 na flash disk yenye thamani ya Sh20,000 na mali nyingi zenye jumla ya thamani ya Sh2.42 milioni.

Baada ya kutiwa hatiani, Mahakama ya Wilaya ya Hai ilimhukumu kifungo cha miaka mitano jela kwa kila kosa, huku adhabu hizo zikiamriwa kutumikiwa kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, tukio hilo lilibainika baada ya mhudumu wa ofisi wa mahakama hiyo, Sara Mwakasitu kufika kazini na kukuta kompyuta, skana na flash disk havipo.

Uchunguzi uliofuata ulibaini dirisha la ofisi lilikuwa limevunjwa na fedha zilizokuwa zimehifadhiwa mahakamani pia zimetoweka.

Jeshi la Polisi lilichukua alama za vidole kutoka dirishani na kwenye meza zilizodaiwa kuguswa na mtuhumiwa. Baadaye, wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi walieleza kuwa alama hizo zilifanana na za Judika.

Katika utetezi wake, Judika alikana kutenda makosa hayo. Alidai kuwa awali alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha kabla ya shtaka hilo kubadilishwa na kuwa la kuvunja jengo na wizi, akisisitiza kuwa hakuwa mhusika wa makosa aliyokuwa akishtakiwa.

Hakuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu akitoa sababu 11, zikiwemo madai kwamba kulikuwa na tofauti kati ya shtaka na ushahidi uliotolewa, ushahidi wa alama za vidole haukuwa wa kuaminika na kwamba alikamatwa kwa misingi ya tuhuma pekee.

Upande wa Jamhuri, uliowakilishwa na Wakili wa Serikali, Julieth Komba, uliunga mkono baadhi ya hoja za mrufani na kuiomba Mahakama iruhusu rufaa hiyo.

Wakili huyo alisema kesi hiyo ilitegemea ushahidi wa mazingira kwa kuwa hakuna shahidi aliyemwona Judika akivunja mahakama au kuiba mali hizo. Pia alisema upande wa mashtaka haukuonyesha utambulisho wa mali zilizoibwa kwa kina wala kueleza mazingira ya kukamatwa kwa mtuhumiwa au kama alipatikana na mali hizo.

Akitoa uamuzi, Jaji Simfukwe alisema ingawa ilithibitika kuwa mali zilizoibwa zilikuwa za Mahakama ya Mwanzo ya Bomang'ombe, ushahidi uliotolewa haukuondoa mashaka kuhusu kuhusika kwa Judika na tukio hilo.

Alisema ushahidi wa alama za vidole, ambao ulikuwa msingi mkuu wa hukumu ya Mahakama ya Wilaya, ulikuwa na dosari kwa kuwa ulifikishwa maabara ya uchunguzi wa kisayansi baada ya kuchelewa bila kutolewa maelezo ya kuridhisha kuhusu ucheleweshaji huo.

Jaji huyo pia alisema hakuna ushahidi mwingine wa kuaminika uliomuunganisha Judika na tukio hilo, wala haukuwasilishwa ushahidi unaoonyesha alipatikana na mali zilizoibwa.

"Kwa kuwa upande wa mashtaka haukuondoa mashaka hayo, hukumu ya kutiwa hatiani haiwezi kusimama," alisema Jaji Simfukwe kabla ya kutengua hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Hai na kuamuru Judika aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.