Aliyekuwa bosi TPA asomewa mashtaka akiwa kitandani Muhimbili

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66).

Muktasari:

  • Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66) amesomewa mashtaka ya kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh4.2 bilioni akiwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66) amesomewa mashtaka ya kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh4.2 bilioni akiwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesomewa mashtaka akiwa kitandani leo Jumatatu Julai 4, 2022 baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo katika hospitali hiyo.

Kesi dhidi yake inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam, Ramadhani Rugemarila

Wakili wa Serikali, Timotheo Mmari alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi ambayo ni la kula njama, kutumia madaraka vibaya na kuisababishia hasara mamlaka hiyo.

Mbali na Kipande, washtakiwa wengine wanne ambao walisomewa mashtaka hayo Juni 30, 2022 Peter Gawile (58), Ofisa Rasilimali Watu wa TPA, Casmily Lujegi (65), Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59), Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Mmari alidai katika shtaka la kwanza kuwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 and Oktoba Mosi, 2020, jijiji Dar es Salaam, washitakiwa wanadaiwa kula njama na kuisababishia TPA hasara.

Alidai kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 washtakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia Dola za Marekani 1,857,908.04.

Ilidaiwa katika shtaka la pili kuwa kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi, 2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washitakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha Bodi ya Zabuni ya TPA.

Alidai uamuzi huo haukufuata kanuni za zabuni, hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8 Sawa na zaidi ya Sh 4.2 bilioni

Mmari alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Kipande ataka haki itendeke

Baada ya hakimu kueleza kuwa hakutakiwa kujibu chochote juu ya shtaka linalomkabili, alimpa nafasi Kipande asema kama ana lolote la kusema ambalo haliusiani utetezi wa kesi.

Kipande: “Sasa mheshimiwia naomba kujua inakuwaje ninafikishwa mahakamani wakati upelelezi haujakamilika?

Hakimu: Suala la upelelezi bado wako kwenye mchakato wa kumaliza na wakati mwingine inategemea na aina ya mashtaka na aina ya kesi.

Kipande: Nategemea hawa wapelelezi watafanya kazi yao bila upendeleo, natumaini haki itatendeka.

Akauliza tena: Sasa kutokana na hali yangu kama hii, nimefanyiwa oparesheni ya mgongo, nitafikaje mahakamani?

Hakimu: Sio lazima uende mahakamani, unaweza kutafuta mawakili wakakuwakilisha vizuri tu.