Aliyekuwa mbunge aapishwa tena

Mbunge mpya wa Mbarali, Bahati Ndingo akila kiapo leo Jumanne Octoba 31, 2023

Muktasari:

Mbunge Ndingo ni sawa na mtu aliyehamisha fedha kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine, ametoka ubunge viti maalumu kuwa mbunge wa jimbo.

Dodoma. Mbunge mpya wa Mbarali, Bahati Ndingo ameapa leo baada ya kushinda nafasi hiyo kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Septemba 19, 2023.

Uchaguzi mdogo wa ubunge Mbarali umefanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega (CCM), kilichotokea Julai mosi, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta dogo (power tiller), kisha kuzikwa Ludewa mkoani Njombe

Ndingo ameapishwa leo Jumanne Oktoba 31, 2023 katika kikao cha kwanza cha Bunge katika Mkutano wa 13.

Kabla ya uchaguzi huo, Ndingo alikuwa ni mbunge wa viti maalumu na alilazimika kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake.

Kwa utaratibu huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi sasa inayo nafasi ya kupeleka bungeni jina la mwanachama mwanamke kutoka CCM ili kuziba pengo lililoachwa na Bahati kwenye ubunge wa viti  maalumu.

Leo wabunge wanawake waliingia na mbunge huyo wakishangilia na kuimba wimbo wa CCM, CCM hadi walipompeleka eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kuapishwa  kisha akaonyesha kiti cha kukaa ambacho ni tofauti na alichokuwa akikitumia awali.

Katika uchaguzi wa Septemba, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbarali, Missana Kwangura amemtangaza Ndingo kuwa mshindi wa kiti cha ubunge wa jimbo hilo baada ya kupata kura 44,334 kati ya kura 56,095 halali zilizopigwa kwenye vituo 490 vya kupigia kura.

Inaelezwa kuwa Ndingo amewashinda wagombea wengine 12 waliokuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge kwenye uchaguzi huo mdogo.

Kwenye uchaguzi huo ushindani mkubwa ulionekana ukiwa baina ya Ndingo na Modestus Kilufi aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, aliyepata kura 10,014.

Akitangaza matokeo hayo Kwangura amesema wapigakura walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Jimbo la Mbarali ni 185,836 kati yao 56,662 ndio waliopiga kura. Ameongeza kuwa kura halali zilikuwa 56,095 na kura zilizokataliwa ni 567.

Wengine waliokuwa wanagombea kwenye kinyang’anyiro hicho ni Halima Abdalah Magambo (AAFP) aliyepata kura 336, Osward Joseph Mndeva (DP) aliyepata kura 130, Zavely Raurent Seleleka (UDP) aliyepata kura 158, Exavery Town Mwataga (CCK) aliyepata kura 118 na Morris Thomas Nkongolo (TLP) aliyepata kura 139.

Wengine ni Mary Moses Daudi (UPDP) aliyepata kura 113, Fatuma Rashidi Ligania (NLD) aliyepata kura 105, Bariki Oswald Mwanyalu (Demokrasia Makini) aliyepata kura 207, Hashim Abasi Mdemu (ADC) aliyepata kura 173, Mwajuma Noty Mirambo (UMD) aliyepata kura 113 na Husseni Hasani Lusewa kutoka Chama cha ADA- TADEA aliyepeata kura 155.