Aliyeonywa kwa Kimakonde, afariki dunia kwa kuangukiwa na jiwe
Muktasari:
- Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe kubwa alipokuwa akichimba mawe kwa ajili ya kuponda kokoto mkoani Mtwara.
Mtwara. Mtu aliyetambuliwa kwa jina la Said Hassan Nampali (60), amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe katika machimbo ya kokoto yaliyopo Kitongoji cha Mbulu Kata ya Mayanga mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 27, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo amesema tukio hilo lilitokea Juni 26 majira ya saa 9 jioni wakati mtu huyo akiwa anachimba mawe kwa ajili ya kuponda kokoto.
“Siku ya tukio marehemu akiwa katika shughuli zake za kuchimba mawe kwa ajili ya kuponda kokoto ghafla jiwe hilo kubwa (jabali) lilianguka na kumkandamiza na baada ya majirani kusikia kishindo kikubwa walisogea eneo hilo na kubaini uwepo mtu chini ya jiwe hilo,” amesema.
Amesema juhudi zilifanyika kwa kushirikiana na wananchi ili kuondoa mwili eneo la tukio na ulipelekwa katika kituo cha afya Mikindani, ambapo uchunguzi wa kitabibu ulibaini kifo hicho kimesababishwa na kuangukiwa na jiwe hilo.
“Natoa wito kwa wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari wanapokuwa wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia usalama kwanza ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya watu,” amesema Katembo.
Akizungumza na Mwananchi katika eneo hilo, mmoja wa washuhuda wa tukio hilo Said Mtepa, amesema alimtahadharisha marehemu kuhusu jiwe hilo wakati anaanza kuchimba na alijibu kuwa amesikia, lakini hakutoka katika eneo hilo.
“Niliona yuko katika hatari kwakuwa jiwe halikuwa na kitu chochote ambacho kimelishikilia nilimwambia kuhusu hilo jiwe na kumwambia asilikalie kati linaweza kumletea madhara akajibu kwa kimakonde kuwa nimekusikia lakini hakutoka katika eneo hilo,” amesema.
Naye Seleman Abdallah mkazi wa kata hiyo, amesema kwamba marehemu alikuwa ndugu yake na alikuwa akifanya kazi ya kuchimba kokoto katika eneo hilo.
“Niliambiwa kuwa ndugu yangu amefunikwa na jiwe kubwa nilifika kwenye tukio na kumkuta akiwa ameangukiwa na jiwe na tayari alikuwa amefariki,” amesema.
Akizungumzia uhalali wa uchimbaji kokoto katika eneo hilo, Meneja Madini Mkowa wa Mtwara, Mhandisi Ephraim Mushi amesema kuwa eneo hilo halina leseni.