Prime
Dawa za tiba tishio jipya vita dhidi ya dawa za kulevya
Muktasari:
- Tofauti na dawa za kulevya zinazozalishwa na kusambazwa kinyume cha sheria, dawa hizi hutengenezwa na kutumika hospitalini kwa ajili ya matibabu ya maumivu makali, matatizo ya usingizi na changamoto za afya ya akili.
Dar es Salaam. Wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa za kulevya, tahadhari mpya imetolewa kuhusu ongezeko la matumizi mabaya ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, ambazo sasa zinatajwa kuwa moja ya changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya uraibu.
Tofauti na dawa za kulevya zinazozalishwa na kusambazwa kinyume cha sheria, dawa hizi hutengenezwa na kutumika hospitalini kwa ajili ya matibabu ya maumivu makali, matatizo ya usingizi na changamoto za afya ya akili.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema matumizi yake yasiyo sahihi yamezifanya kuwa chanzo kipya cha uraibu nchini na duniani.
Dawa zinazotajwa kuwa katika kundi hilo ni pamoja na Pethidine, Morphine, Tramadol, Valium, Fentanily na nyingine zinazotolewa kwa wagonjwa chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya.
Wadau wa afya na udhibiti wa dawa za kulevya
Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2025, dawa zinazotengenezwa kwa ajili ya matibabu zimeendelea kuchangia ongezeko la uraibu na madhara ya kiafya pale zinapotumiwa bila usimamizi wa kitabibu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa matumizi yasiyo ya kitabibu ya dawa aina ya Tramadol, yameongezeka kwa kasi katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi na Kati kupitia mifumo isiyo rasmi ya usambazaji.
Aidha, dawa zenye msingi wa ‘codeine’ na ‘diazepam’ zimekuwa zikichepushwa kutoka katika mfumo rasmi wa afya na kuingia katika masoko yasiyodhibitiwa.
Ketamine nayo imeendelea kutajwa katika ripoti hiyo kutokana na matumizi yake yasiyo ya kitabibu katika baadhi ya nchi za Asia na Ulaya.
Wataalamu wanaonya kuwa matumizi ya muda mrefu ya dawa hiyo, yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya mfumo wa mkojo pamoja na changamoto za afya ya akili.
Hali hiyo imeonekana pia nchini Tanzania. Takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka 2025 jumla ya waraibu 62,926 walipatiwa huduma za matibabu na urekebishaji tabia, ambapo wanaume walikuwa 46,464 na wanawake 16,462.
Miongoni mwa waliopatiwa huduma hizo walibainika kutumia pombe, bangi, mirungi, heroini na kokeni, huku wengine wakitumia dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Akizungumzia hilo, Kamisha Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo anakiri kuwa tatizo ni kubwa akieleza kuwa kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya za viwandani, kumechangia baadhi ya waraibu kugeukia dawa hizi za hospitali kama mbadala wa dawa haramu.
“Tatizo ni kubwa kwa sababu watu wengi waliokuwa wanatumia dawa za kulevya ikiwemo heroini, kokeni sasa wanapokosa wanatafuta hizi dawa tiba za kulevya. Wafanyabiashara wanazichanganya dawa hizi na vitu vingine na kuwaamisha watumiaji kuwa ni heroini, matokeo yake mtu anapotumia tu anapata madhara makubwa ikiwemo vifo vya ghafla.
“Ila habari njema ni kwamba dawa hizi kwa sasa tunakwenda kuziingiza kwenye sheria, ukikamatwa nazo bila taarifa ya daktari utachukuliwa hatua kama umekutwa na dawa za kulevya.Kumekuwa na udhibiti mkubwa wa utoaji wa dawa hizi kwa matumizi ya matibabu,”
Athari kiafya
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Christopher Maina, anasema dawa hizo zina uwezo mkubwa wa kuathiri mfumo wa fahamu wa binadamu na hivyo zinahitaji matumizi ya uangalizi wa karibu wa kitabibu.
Anasema dawa nyingi zinazotumika kutibu maumivu makali, matatizo ya usingizi au changamoto za afya ya akili, huwa na kemikali zinazoweza kusababisha uraibu endapo zitatumiwa bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
“Tatizo kubwa si dawa zenyewe, bali namna zinavyotumiwa. Watu wengine huongeza dozi kwa hiari yao wakiamini zitatoa athari kubwa zaidi. Hapo ndipo hatari ya uraibu inaanza,” anasema Maina.
Anasema kwa mfano, mgonjwa anayepatiwa Tramadol kwa matibabu anaweza kupewa kati ya miligramu 50 hadi 100 mara mbili au tatu kwa siku kwa muda maalumu, lakini baadhi ya watumiaji hutumia hadi miligramu 500 au 1,000 kwa siku kwa lengo la kujifurahisha.
“Unapoongeza dozi bila ushauri wa daktari au kutumia dawa kwa muda mrefu kuliko ulivyoshauriwa, unabadilisha namna ubongo unavyofanya kazi na hatimaye unaweza kuingia kwenye uraibu,” anasema.
Mtaalamu wa afya ya jamii, Luisa Mashauri, anasema matumizi ya muda mrefu ya dawa hizo kwa kiwango kikubwa, yanaweza kusababisha madhara katika figo, ini na mifumo mingine muhimu ya mwili.
Anasema wagonjwa wengi huanza kutumia dawa hizo kwa sababu halali za matibabu, lakini baadaye huendelea kuzitumia bila usimamizi wa daktari hadi kufikia utegemezi wa dawa hizo.
“Matumizi ya dawa hizi bila kufuata maelekezo ya kitabibu yanaweza kuleta madhara yanayofanana na yale yanayosababishwa na dawa za kulevya. Mtu anaweza kujikuta hawezi kufanya shughuli zake za kawaida bila kutumia dawa hizo,” anasema Mashauri.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika Profesa Mohamed Janabi wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) aliwahi kueleza kuwa dawatiba zenye asili ya kulevya zinapotumika bila maelekezo ya daktari, zinaathiri mwili wa binadamu na kumsababishia madhara ya kiafya, ikiwemo magonjwa ya moyo, figo, saratani na vifo vya ghafla.
"Dawatiba wanazotumia sisi kule hospitali tunatumia kumlaza mgonjwa kabla ya kumpeleka chumba cha upasuaji. Sasa dawa ya aina hii inavyotumika ovyo hata sisi wenyewe hatuelewi kinachotengenezwa ni nini huko mwilini,’’ anasema na kuongeza:
"Dawa hizi zinaingiliana na mfumo wa umeme wa moyo, ndiyo maana siku hizi kuna matukio mengi ya vifo kwa vijana wanaotumia dawa hizi, utasikia wame-overdose, ukweli ni kwamba mfumo wa umeme moyo unakuwa umeingiliwa.