Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yatakiwa kuongeza uwekezaji utoaji huduma za afya ya akili 

Katibu wa Serikali anayeshughulikia Afya ya Akili nchini Ushelisheli, Bonyl Naiken.

Muktasari:

  • Afrika yaonywa kuongeza uwekezaji wa afya ya akili kutokana na uhaba wa wataalamu, fedha na huduma, hali inayoweza kuzuia kufikia malengo yaliyokusudiwa ifikapo 2030.

Dar es Salaam. Nchi za Afrika zimetakiwa kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya akili, kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata matibabu na msaada wa kisaikolojia, vinginevyo bara hilo litashindwa kufikia malengo ya afya ya akili ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Juni 25, 2026 wakati wa Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Afya PEN-Plus unaofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 23 hadi 25, 2026, ambao unalenga kusogeza huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza karibu na wananchi kupitia hospitali za wilaya na mikoa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mataifa ya Afrika yanaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Afya ya Akili wa mwaka 2013 hadi 2030 kupitia mfumo wa kikanda uliopitishwa mwaka 2022 unaolenga kuimarisha uongozi, sera, sheria na ufadhili wa huduma hizo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa WHO na daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Chido Ratidzai, amesema takribani watu milioni 150 Afrika wanaishi na changamoto za afya ya akili, lakini eneo hilo bado linapokea rasilimali chache katika mifumo ya afya.

Amesema afya ya akili haiwezi kutenganishwa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, wala mjadala wa magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa changamoto hizo zina uhusiano mkubwa.

“Hatuwezi kuzungumzia magonjwa yasiyoambukiza bila kuzungumzia afya ya akili. Afya ya akili si anasa bali ni haki ya msingi ya binadamu na sehemu muhimu ya afya kwa ujumla,” amesema.

Dk Ratidzai amesema msongo wa mawazo, sonona, matumizi ya dawa za kulevya na pombe ni miongoni mwa sababu zinazoongeza mzigo wa magonjwa katika bara hilo.

Amesema Afrika bado ina kiwango cha juu cha vifo vinavyotokana na kujiua duniani, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika huduma za kinga, tiba na msaada wa kisaikolojia.

Mbali na changamoto za fedha, bara hilo pia linakabiliwa na uhaba  wa wataalamu wa afya ya akili, Dk Ratidzai amesema kwa wastani kuna daktari mmoja bingwa wa magonjwa ya akili anayehudumia watu 100,000.

Ameongeza wataalamu wengine wa afya ya akili wakiwemo wanasaikolojia, wauguzi wa afya ya akili, wataalamu wa ustawi wa jamii na tiba kazini ni wastani wa watu 2.2 pekee kwa kila watu 100,000.

“Katika baadhi ya nchi, wataalamu ni wachache sana na wanahudumia mamilioni ya wananchi, jambo linalochelewesha uchunguzi na matibabu,” amesema.

Amesema changamoto nyingine ni upatikanaji mdogo wa dawa za afya ya akili katika vituo vya msingi vya afya, huku nchi 10 pekee katika ukanda wa Afrika wa WHO zikiripoti kuwa na upatikanaji endelevu wa dawa hizo.

Kwa upande wake, Katibu wa Serikali anayeshughulikia Afya ya Akili nchini Ushelisheli, Bonyl Naiken, amesema Afrika inapaswa kuondoka kwenye hatua ya kuandaa sera na kuanza kuzitekeleza kwa vitendo.

Amesema afya ya akili si suala la afya pekee bali linahusisha haki za binadamu, maendeleo ya jamii na uchumi.

“Hakuna afya bila afya ya akili, na hakuna maendeleo endelevu bila kuwekeza katika ustawi wa akili wa wananchi wetu,” amesema.

Naiken amesema uwekezaji katika afya ya akili unapaswa kuonekana kama uwekezaji katika uzalishaji, elimu, mshikamano wa kijamii na ustahimilivu wa uchumi.

Ametaja maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele kuwa ni kuimarisha uongozi, kuongeza fedha za huduma za afya ya akili, kuunganisha huduma hizo katika mfumo wa afya kwa ujumla, kuongeza wataalamu na kuwekeza katika kinga na uhamasishaji.

Naye mwanaharakati wa afya ya akili na mraibu wa zamani wa pombe kutoka Zimbabwe, Jacob Shamuyarira (54), amesema ni muhimu kuunganisha huduma za afya ya akili na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema alitumia pombe kwa miaka 15 na kupoteza mwelekeo wa maisha kabla ya kuacha, ambapo sasa ametimiza miaka 10 tangu kuondokana na uraibu huo.

Shamuyarira amesema uzoefu wake umeonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi mabaya ya pombe, matatizo ya afya ya akili na magonjwa sugu kama shinikizo la damu.

Amesema unyanyapaa na ubaguzi bado ni vikwazo vikubwa vinavyowafanya watu wengi kushindwa kutafuta msaada mapema.

Amehimiza serikali kuimarisha sera za kudhibiti matumizi ya pombe na kuelekeza sehemu ya mapato yatokanayo na kodi za vileo katika huduma za kinga na matibabu ya afya ya akili.

WHO inaonyesha uwekezaji katika afya ya akili Afrika bado ni mdogo, ambapo matumizi kwa kila mtu ni dola za Marekani 0.07 pekee ikilinganishwa na wastani wa dunia wa dola 2.5.

Aidha, Afrika ina wataalamu 2.2 wa afya ya akili kwa kila watu 100,000, tofauti na wastani wa dunia wa wataalamu 13.5 kwa kila watu 100,000.

Takwimu hizo zinaonyesha pengo kubwa la huduma ambalo linaendelea kuchangia mzigo wa changamoto za afya ya akili katika bara hilo.