Aliyeshikiliwa kumlawiti mwanae wa miaka mmoja kizimbani akidaiwa kulawiti mtoto wa miaka 9
Iringa. Mkazi wa Kijiji cha Nzihi aliyewahi kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa kwa tuhuma za kumlawiti mwanae wa mwaka mmoja na miezi kumi amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa, zamu hii akidaiwa kumlawiti mtoto wa kufikia wa miaka 9.
Amani Martin (47) anadaiwia kufanya unyama huo katika nyumba ambayo anaishi na mke wake na mtoto huyo.
Takribani wiki moja Iliyopita Jeshi la Polisi mkoani humo lilitangaza kumshikilia Martin, maarufu kama Kasisi, akituhumiwa kumlawiti mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.
Inadaiwa kuwa April 4, 2023 mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake nje ya nyumba yao na baadae akaingia ndani kwa ajili ya kunywa maji ndipo inadaiwa Amani Martini kumfanyia kitendo hicho cha ukatili wakati mkewe akiwa sokoni.
Baada ya kumaliza kumfanyia ukatili huo inadaiwa mtuhumiwa huyo alimtishia mtoto huyo kutotoa taarifa hiyo.
Hata hivyo baada ya kuwa na maumivu mtoto huyo alimwambia mama yake ndipo taratibu za kumpeleka hospitalini zikafanyika.
Wakati upelezi ukiendelea Jeshi la Polisi lilibaini kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kutenda kosa hilo kwa mtoto wa mke wake mwenye umri wa miaka 9 tuhuma ambazo zimemfikisha jana mahakamani hapo.
Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka hayo amekana kufanya tukio hilo, kesi imeahirishwa jana ambapo inatarajiwa kuendelea kusikiliza hii leo.
Kesi hiyo imesomwa April 19,2023 mbele ya Hakimu Mwandamizi, Emmy Msangalufu wa Mahakama hiyo ya Wilaya ikiwa na mashahidi 7 na kielelezo kimoja.