Aliyevunja Kanisa Katoliki Geita jela miaka mitatu

Elpidius Edward  (aliyevaa fulana nyeupe) mkazi wa Mtaa wa Katundu Mjini Geita aliyehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, kwa kosa la kufanya uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni mali ya Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita.

Muktasari:

  • Kesi hiyo namba 62 ya mwaka 2023 ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 6, 2023 na mshitakiwa akidaiwa kutenda kosa la kuvunja na kuingia kwenye Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita akiwa na dhumuni la kufanya kosa la kuharibu mali Februari 26, 2023

Geita. Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imemtia hatiani Elpidius Edward mkazi wa Mtaa wa Katundu Mjini Geita na kumuhukumu kwenda jela miaka mitatu, kwa kosa la kufanya uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni mali ya Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Januari 16, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Johari Kijuwile baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka katika shitaka la pili lililokuwa linamkabili mshitakiwa.

Hakimu Kijuwile ameieleza Mahakama mshitakiwa alikuwa akishitakiwa kwa makosa mawili, likiwemo la kuingia katika jengo la Kanisa Katoliki Geita kinyume na kifungu cha 294 (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shitaka la pili, mshitakiwa alishtakiwa kwa kosa la kuharibu mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni kinyume na kifungu namba 226 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kijuwile amesema Mahakama imemtia mshitakiwa hatiani kwa kosa la pili la kuharibu mali kwa nia ovu,  na upande wa mashitaka umethibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mali zilizoharibiwa zilikuwa mali ya Kanisa Katoliki Geita .

Amesema  mshitakiwa kwenye mahojiano yake na Polisi alikiri kuharibu mali ya kanisa na wakati wa utetezi akihojiwa na upande wa mashitaka hakudai kupigwa na Polisi, hivyo ni dhahiri alikiri kutenda kosa lile yeye binafsi mbele ya Polisi bila kulazimishwa.

Ameieleza Mahakama kuwa kwa taarifa iliyotolewa na daktari mahakamani hapo mshitakiwa alikua na akili timamu,  hivyo Mahakama imejiridhisha pasi kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa la kuharibu mali za kanisa kwa makusudi.

Kuhusu kosa la kwanza hakimu amesema  hati ya mashtaka imeeleza kosa la kuvunja jengo kinyume na kifungu namba 264(1) na (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu, lakini kifungu hicho hakizungumzii uvunjaji wa jengo kama kinavyozungumzwa bali kinazungumzia uvunjaji wa nyumba usiku.

Hakimu ameieleza Mahakama hati ya mashitaka haielezi muda ambao mshitakiwa amefanya kosa hilo kama ni mchana au ni usiku na kuwa ni lazima mlalamikaji aelewe maelezo ya kosa ndio yanayojenga shitaka na yanapokuwa tofauti yanaweka kiwingu,  kinachoweza kuleta wasiwasi na kufanya mshitakiwa anufaike.

Hakimu Kijuwile amesema kuwa kwenye hati ya mashitaka imeeleza tofauti na tukio lilivyokuwa na kutokana na hilo upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kosa pasi kuacha shaka. Hivyo Mahakama imemtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la pili.

Wakili wa Jamhuri, Scolastika Teffe ameiomba Mahakama licha ya kuwa mshitakiwa hana makosa aliyoyafanya nyuma impe adhabu kali ili iwe fundisho.

Akitoa ombolezo mshitakiwa ameiomba Mahakama kumuachia huru kwa kuwa ni mgonjwa wa kifua kikuu na familia yake ni change. Pia amejitetea kuwa  amelelewa kwenye imani ya Kanisa Katoliki hivyo asingeweza kutenda kosa kama hilo kwa makusudi.