Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amani, mazingira bora ya kisiasa kubeba mpango wa maendeleo wa Taifa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wkati akiwasilisha taarifa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Alhamis Juni 11, 2026. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Maeneo haya 10 yanatajwa kuwa nguzo ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Dar es Salaam. Serikali imetaja maeneo 10 yatakayobeba utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27, ikisema mafanikio ya mpango huo yatategemea uwepo wa mazingira bora ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yatakayowezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa.

Akizungumza wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Juni 11, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali imeweka misingi muhimu itakayohakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Profesa Mkumbo amesema eneo la kwanza ni kuendelea kuwepo kwa demokrasia, amani, usalama na utulivu ndani ya nchi na katika mataifa jirani ili kuwezesha shughuli za kiuchumi, kijamii na uwekezaji kustawi.

Amesema eneo la pili ni kudumisha misingi ya utawala bora na wa sheria, ikiwemo uwajibikaji, uadilifu, uwazi na matumizi bora ya rasilimali za umma.

“Utekelezaji wa mpango huu unahitaji mazingira ya utawala yanayojenga imani kwa wananchi na wawekezaji pamoja na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija,” amesema.

Eneo lingine ni kuendeleza miundombinu wezeshi ikiwemo nishati, bandari, barabara na reli ili kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha biashara, viwanda na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Amesema matumizi ya teknolojia za kidijitali katika uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii ni eneo lingine litakalobeba utekelezaji wa mpango huo.

“Pia Serikali itaendelea kutekeleza mageuzi ya kitaasisi na kiutawala yanayoongozwa na falsafa ya 4R ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma,” amesema.

Profesa Mkumbo amesema kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni eneo lingine litakaloangaliwa.

Hilo litaenda sambamba na kutumia fursa zinazotokana na ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kuendelea kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na yasiyo ya asili, milipuko ya magonjwa, migogoro ya kikanda pamoja na misukosuko ya kiuchumi duniani pia itaangaliwa kwa umakini.

“Pia Serikali inatarajia kuendelea kusimamia kuhakikisha kunakuwapo na kuimarika kwa uchumi wa dunia pamoja na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa, hali ambayo itasaidia utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo,” amesema.

Haya yote yatafanyika wakati ambao uimarishaji na upatikanaji na usalama wa chakula nchini utazingatiwa jambo ambalo linatajwa kuwa muhimu kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi.

“Eneo la mwisho ni kuhakikisha kuna mifumo thabiti ya uratibu, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya programu, miradi na afua zote zilizopangwa ili zitekelezwe kwa wakati na kuleta matokeo yaliyokusudiwa,” amesema.

Haya yote yatafanyika kwa kushirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi kuhakikisha maeneo hayo yanatekelezwa kwa ufanisi ili kuharakisha maendeleo ya Taifa na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.