Amuua mkewe akimtuhumu kutumia ARV kwa siri

Amuua mkewe akimtuhumu kutumia ARV kwa siri

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia, Peter Elias (29) mkazi wa Ndembezi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mkewe, Pili Luhende akimtuhumu kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kwa siri.

Shinyanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia, Peter Elias (29) mkazi wa Ndembezi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mkewe, Pili Luhende akimtuhumu kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kwa siri.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 7, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea  Mei 3, 2021 katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi.

Amesema mtuhumiwa alimpiga Pili maeneo mbalimbali mwilini na alipobaini amefariki dunia, aliuchukua mwili wake na kwenda kuutupa maeneo ya daraja la Mwagala.

"Baada ya taarifa hiyo mtuhumiwa tulimkamata na kumhoji ambapo jana alionyesha alipoutelekeza mwili wa marehemu maeneo ya Mwagala darajani.”

“Baada ya kuhojiwa alibainisha kuwa alimpiga kwa ngumi chanzo kikiwa ni mtuhumiwa kumbaini mkewe anatumia dawa ARV kwa kificho jambo lililomkasirisha  na pia alisema walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara,” amesema kamanda huyo.

Amesema mwili ulikutwa ukiwa umeharibika na ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.