Anayedaiwa kuua mama na mtoto wake akamatwa

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Alex Mkama akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 27, 2023. Lilian Lucas.

Muktasari:

  • Kijana anayedaiwa kufanya mauaji ya mama na mwanaye anashikiliwa na polisi, inadaiwa alivitupa vichwa vya wawili hao mtoni.

Morogoro. Polisi mkoani Morogoro imemkamata Seleman Mabula Sita (25), mkazi wa Seke mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya mama na mtoto ake kwa kuwakata vichwa na kutenganisha na viwiwili.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kukamatwa akiwa katika harakati za kutoroka, akiwa kwenye basi la abiria lilikuwa likielekea mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama amesema hayo leo Novemba 27, 2023 alipozungumza na waandishi wa habari juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea mkoani hapa.

Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo alifanya mauaji hayo Novemba 24, 2023 muda wa alfajiri katika Kitongoji cha Ilangali, Kijiji cha Mavimba, Kata ya Milola Wilaya ya Ulanga.

Anadaiwa katika tukio hilo aliwaua Mwanaisha Matele (37) na mtoto wake Baraka Maita (7), mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mavimba.

Baada ya mtuhumiwa kukamatwa, imeelezwa alikwenda kuonyesha polisi alikotupa vichwa hivyo katika Mto Ulala. Mpaka sasa mtuhumiwa hajaeleza sababu za kufanya mauaji hayo.

Amesema uchunguzi unaendele ili hatua zaidi za kisheria zichukuliea dhidi ya mtuhumiwa.

“Natoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kupokea na kuwahifadhi wageni ambao hawawafahamu na badala yake watoe taarifa kwa viongozi wa Serikali za mitaa ama vijiji pindi wanapokuja, ili wahojiwe na kufuatiliwa mienendo yao kabla ya kufanya matukio ya uhalifiu,” amesema.

Inadaiwa mtuhumiwa alifika na kuishi katika familia ya Juma Maita (baba wa familia) kwa ajili ya kutafuta mashamba ya kulima na alikaa hapo wiki mbili na alifanya mauaji hayo wakati baba wa familia akiwa safarini mkoani Dodoma.

Wakati huohuo, polisi linamtafuta mtu mmoja kwa tuhuma za kufanya mauaji ya Audi Mlozi (38) aliyekuwa na tatizo la afya ya akili kwa kumchoma kisu.

Amesema mtuhumiwa huyo mkazi wa Mji Mwema Wilaya ya Morogoro, alimchoma kisu mwenzake baada ya kutokea ugomvi na marehemu.

Mkama amesema kwa sasa polisi inafanya jitihada za kumtafuta mtu huyo, kwani anafahamika na akipatikana atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabiliili viweze kukabiliana na mkondo wake.